
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi wiki hii WHO ilisisitiza mchango wa muda mrefu wa Marekani kama mwanachama mwanzilishi, ikiwa ni pamoja na mafanikio makubwa ya afya ya dunia kama vile kutokomeza ugonjwa wa ndui na kupiga hatua dhidi ya polio, VVU, Ebola, malaria na magonjwa mengine hatari.
Shirika hilo limesema “WHO kwa hiyo inajutia notisi ya Marekani ya kujiondoa katika WHO uamuzi unaofanya Marekani na dunia kuwa katika hali isiyo salama zaidi,” likiongeza kuwa suala hilo litajadiliwa rasmi katika kikao cha Bodi Kuu ya WHO mwezi Februari na katika Baraza la Afya Duniani WHA mwezi Mei 2026.
WHO yakanusha madaia ya upendeleo na kutokua huru
WHO pia imejibu madai ya Marekani kwamba shirika hilo “limechafuliwa na kudhalilishwa na kupoteza uhuru wake, ikiyapinga vikali madai hayo.
Shirika hilo limesema limekuwa likishirikiana na Marekani “kwa nia njema, kwa heshima kamili ya mamlaka yake ya kitaifa,” likisisitiza kuwa kutokuwa na upendeleo ni msingi wa jukumu lake kama Shirika maalum la Umoja wa Mataifa linaoongozwa na Nchi Wanachama 194.
“Kinyume chake ndicho kilicho kweli,” WHO imesema, ikibainisha kuwa “ipo kuhudumia nchi zote, kwa heshima ya mamlaka zao za kitaifa, bila hofu wala upendeleo, na haifuati ajenda yoyote ya kisiasa”.
WHO yatetea hatua zake dhidi ya COVID-19 na tahadhari za mapema
WHO pia imekanusha madai ya Marekani kwamba ilishindwa wakati wa janga la coronavirus“>COVID-19 au ilizuia ushirikishaji wa taarifa muhimu.
Ingawa ilikiri kuwa “hakuna shirika wala serikali iliyofanya kila kitu kikamilifu,” WHO imesisitiza kuwa ilisimama imara katika hatua zake, ikisema ilichukua hatua “haraka, kwa uwazi, na kwa kuzingatia ushahidi bora uliokuwepo.”
WHO ilitangaza COVID-19 kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa tarehe 30 Januari 2020, wakati kulikuwa na chini ya visa 100 vilivyoripotiwa nje ya China na hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Katika wiki za awali, Mkurugenzi Mkuu wa WHO aliwataka mara kwa mara viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka, akionya kuwa “dirisha la fursa linafungwa,” akisisitiza kuwa “hili si zoezi, na kuutaja ugonjwa huo kama adui wa umma namba moja.”
Mageuzi yaongeza uwezo wa dunia kukabiliana na majanga
Kufuatia tathmini kadhaa huru kuhusu janga hilo, WHO imesema imeimarisha mifumo yake na kusaidia nchi kuimarisha uwezo wao wa kujiandaa na kukabiliana na majanga ya afya.
Shirika hilo limesisitiza kuwa “mifumo yake ya dharura inafanya kazi saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki, na imechangia kulinda nchi zote, ikiwemo Marekani.”
WHO pia imefafanua kuwa, ingawa ilipendekeza matumizi ya barakoa, chanjo na umbali wa kimwili, “haikuwahi kupendekeza maagizo ya lazima ya kuvaa barakoa, chanjo au kufungwa kwa shughuli,” ikibainisha kuwa maamuzi yote yalikuwa chini ya mamlaka ya serikali husika.
Wito kwa Marekani kurejea ushirikiano
Licha ya notisi ya kujiondoa, WHO imesema inaendelea kujitolea kwa ushirikiano wa kimataifa na ikaeleza matumaini kuwa Marekani itarejea kushiriki kikamilifu katika siku zijazo.
Shirika hilo limebainisha mafanikio ya hivi karibuni, ikiwemo kupitishwa kwa Mkataba wa WHO wa Kukabiliana na Majanga, uliotajwa kama “nyenzo muhimu ya kihistoria ya sheria za kimataifa” kwa lengo la kuifanya dunia iwe salama zaidi dhidi ya majanga yajayo.
“WHO inaendelea kujitolea kikamilifu kufanya kazi na nchi zote katika kutimiza dhamira yake kuu,” imehitimisha taarifa hiyo huku, ikithibitisha tena jukumu lake la kikatiba la kuhakikisha “kiwango cha juu zaidi cha afya kinachowezekana kama haki ya msingi kwa watu wote.”