Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limefanya mjadala wa ngazi ya juu leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kuhusu utawala wa sheria wa kimataifa huku onyo kali likitolewa kwamba hali ya kimataifa ya utawala wa sheria inakumbwa na mapungufu na Katibu Mkuu António Guterres akionya kwamba “sheria za msituni zinachukua nafasi ya kanuni za dunia zilizokubaliwa”.

Mjadala huo, uliopewa kichwa cha habari Kuthibitisha upya hali ya sheria ya kimataifa: mikakati ya kuhuisha amani, haki na ushirikiano wa kimataifa,” umekuwa tukio kuu la urais wa Somalia katika Baraza la Usaama na umeangazia njia za kurekebisha ukiukaji wa sheria unaoongezeka na unaohatarisha uthabiti wa dunia.

Hali ya sheria inachukuliwa kama menu ya chakula

Akihutubia mjadala huo wa Baraza la Usalama, Bwana. Guterres amesema hadhi ya sheria za kimataifa inashushwa chini katika migogoro na maeneo kadhaa duniani.

“Kutoka Gaza hadi Ukraine, kutoka Sahel hadi Myanmar na Venezuela, hali ya sheria leo inachukuliwa kama menu ya kula kwa chaguo,” amesema Guterres, akionya kwamba utekelezaji wa kuchagua ni chanzo cha kutokuwepo kwa usawa na kudhoofisha uthabiti.

Miaka themanini baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mfumo wa kimataifa uko katika kipingamizi cha hatua.

“Baraza la Usalama lazima lioneshe njia,” amesema, akisisitiza kuwa mageuzi ya Baraza ni “ya lazima kurejesha uaminifu na ufanisi”.

Ukiukaji unaunda mifano hatari

Katibu Mkuu ametaja mfululizo wa ukiukaji utawala wa sheria unaodhoofisha misingi ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na “matumizi haramu ya nguvu, mashambulizi ya miundombinu ya kiraia, ukiukaji wa haki za binadamu, mabadiliko yasiyo ya kikatiba ya serikali, uzalishaji haramu wa silaha za nyuklia, na kukataliwa msaada muhimu wa kibinadamu”.

Guterres ameonya kuwa “Ukiukaji huu unaunda mifano hatari, ukihimiza nchi nyingine kuchukua hatua kwa maslahi yao wenyewe”.

Amethibitisha kuwa yuko tayari kusaidia Baraza kupitia juhudi za kidiplomasia na upatanisho.

“Kupitia utendaji wangu na juhudi zisizo na kikomo za wajumbe na wadau wa Umoja wa Mataifa, nipo tayari kusaidia Baraza hili kuendeleza hali ya sheria na kujenga dunia salama na thabiti kwa wote,” amesema.

Afrika yataka ushirikiano wa kimataifa unaoaminika

Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf, akizungumza katika mjadala huo amesisitiza wasiwasi wa Katibu Mkuu, akisema kwamba “hali ya sheria ndiyo msingi wa amani.”

Amebainisha kwamba Afrika inazidi kutegemea mifumo ya kisheria, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na mahakama za kikanda, ili kutatua migogoro ishara ambayo amesema bara linaamini sheria lazima itawale badala ya nguvu.

Wakati huo huo, amelaumu ukosefu wa Afrika wa wawakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama.

Amesema “Bara lenye nchi 54 bado halina sauti ya kudumu katika maamuzi yanayoamua mustakabali wake,” ametaka “ushirikiano wa kimataifa unaoweza kuaminika na ulio jumuishi.”

Somalia: Kanuni za Chata ya UN ziheshimiwe

Mwakamilishi wa Kudumu wa Somalia kwenye Umooja wa Mataifa ambaye ndiye Rais wa Baraza Kuu kwa mwezi huu katika mjadala huo amesema  “Mpangilio wa kimataifa hauwezi kuwepo wakati usawa unachukuliwa kama kipaumbele badala ya haki kamili”
Akibainisha kuwa hali ya sheria ni jiwe la msingi la ushirikiano wa kimataifa, mwakilishi huyo ametaka kuimarisha mfumo wa sheria wa kimataifa unaounga mkono hali hiyo.

Amesisitiza kuwa “Ni lazima tuunde dunia ambapo ushirikiano wa kimataifa unaimarishwa badala ya kudhoofishwa, na ambapo uhuru na utu wa nchi unaheshimiwa kwa vitendo.”

Ameongeza kuwa “Tunachohitaji leo ni utashi wa kisiasa wa kutekeleza kanuni hizi kwa uthabiti na bila kupendelea upande mmoja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *