Katika ripoti iliyotolewa leo huko Port-au-Prince na Santo Domingo, ziara ya ngazi ya juu ya shirika hilo imesisitiza kuwa uhakika wa chakula ni changamoto ya pamoja inayohitaji hatua za haraka za kutoa msaada wa kibinadamu na kutengeneza mifumo imara ya kujiandaa na majanga.

Nchini Haiti, ambapo zaidi ya watu milioni 5.7 wanakabiliwa na njaa kali, FAO imefanikiwa kusaidia zaidi ya wakulima 76,000 kuzalisha tani 7,500 za chakula ndani ya siku 90 pekee. Jitihada hizi zimeleta matumaini kwa familia ambazo maisha yao yanategemea kilimo, huku shirika hilo likitafuta dola milioni 108 zaidi ili kuwafikia watu wengine 860,000 nchini humo kupitia uzalishaji wa dharura wa chakula.

Kwa upande wa Jamhuri ya Dominika, FAO imepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa viumbehai na kulinda mifugo dhidi ya magonjwa yanayoambukiza maeneo ya mipakani. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shirika hilo limefanikiwa kuongeza uzingatiaji wa kanuni za usalama kwenye mashamba ya nguruwe kutoka asilimia 35 hadi karibu 80, jambo lililosaidia kulinda soko la biashara ya nguruwe, ndani na nje ya nchi.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, amebainisha kuwa uwekezaji katika sekta ya kilimo si jambo la hiari bali ni msingi wa utulivu na usalama wa chakula kwa nchi zinazokabiliwa na majanga ya mara kwa mara. 

“Baada ya kusafiri kwenye nchi zote mbili, nina hakika kilimo sio tu njia ya maisha katika migogoro ya leo, ndio msingi wa utulivu na uhakika wa chakula. Nchini Haiti, ambapo familia huvumilia mishtuko ya kikatili isiyokoma, kilimo kinasalia kuwa nanga ya kila siku inayoendeleza kaya na ni mbegu kwa ajili ya kujenga upya maisha yanayostahimili,” amesema Bechdol.

Ili kupata matokeo Chanya, hatua hizi jumuishi zinalenga kuhakikisha rasilimali za chakula zinalindwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za minyororo ya usambazaji katika ukanda mzima wa Karibiani.

“Inahitajika kuongeza ufadhili na usaidizi wa haraka ili kuruhusu FAO kuokoa maisha na utu kwa kupata matokeo yenye mashiko kwa wakulima na jamii,” amesema Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Ustahimilivu ya FAO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *