
Katika ujumbe wake mahsusi kwa siku hii Guterres amesema sayansi inaonesha dunia kwa muda sasa inaelekea kuvuka kiwango muhimu cha ongezeko la joto duniani la nyuzi 1.5C. Wajibu uliopo sasa ni kuhakikisha uvukaji huo unakuwa “mdogo kadri iwezekanavyo, wa muda mfupi, na salama kwa kuharakisha mpito wa haki, uliopangwa na wenye usawa kutoka kwenye nishati ya mafuta ya kisukuku. Na Kiini cha mpito huo ni nishati safi au jadidifu”.
Katibu Mkuu ameeleza kuwa nishati jadidifu ni“injini inayoweza kuendesha mpito huu.”
Amesema Upepo, jua na vyanzo vingine safi sasa ni chanzo cha umeme wa gharama nafuu zaidi katika maeneo mengi ya dunia na kwa mara ya kwanza mwaka jana, vyanzo hivi vilizalisha umeme mwingi zaidi duniani kuliko makaa ya mawe.
Faida ni zaidi ya kupunguza hewa ukaa
Amesisitiza kuwa athari zake chanya ni zaidi ya kupunguza hewa ukaa“Nishati jadidifu inaunganisha jamii ambazo bado ziko gizani, inatoa nishati safi ya kupikia, inafungua fursa za afya bora na elimu, inaunda ajira zenye staha, inapunguza gharama za nishati huku ikiilinda nchi dhidi ya misukosuko ya kisiasa ya kimataifa na kuyumba kwa masoko.”
Licha ya hatua hizi, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa mapinduzi ya nishati safi hayasongi kwa kasi ya kutosha. Miundombinu ya gridi ya umeme inasalia nyuma ya upanuzi wa uwezo wa nishati jadidifu, na gharama kubwa bado zinaacha nchi nyingi zinazoendelea nje ya mpito huu.
Hata hiyo amesisitiza suluhisho lipo wazi“Ni lazima tuongeze mara tatu uwezo wa nishati jadidifu duniani ifikapo mwaka 2030 kwa kiwango, kasi, na mshikamano.”
Amesema hii inamaanisha serikali kuunda sera zinazothamini nishati safi na kuharakisha utoaji wa vibali, makampuni ya umeme kuboresha na kuingiza gridi kwenye mifumo ya kiditijitali, na sekta ya viwanda kubadilisha minyororo ya usambazaji ikiwemo madini muhimu ili nchi na jamii zinazozalisha zinufaike, si masoko ya kimataifa pekee.
Fedha zina jukumu muhimu
Ameongeza kuwa fedha pia zina jukumu muhimu.“Gharama ya mtaji lazima ipunguzwe, hasa kwa nchi zinazoendelea zenye uwezo mkubwa wa nishati jadidifu.”
Zaidi ya yote, amesisitiza mpito huu lazima uwe wa haki“Muhimu zaidi, lazima tuhakikishe mpito huu ni wa haki tukilinda wafanyakazi na jamii, na kuunda fursa kwa wote.”
Ujumbe wake wa mwisho ni wa dharura na matumaini akisema Mustakabali wa nishati safi uko ndani ya uwezo wetu. Tuchukue hatua sasa na tupeleke mapinduzi ya nishati jadidifu katika kila pembe ya dunia.”