Mchezo wa ngumi za kulipwa umeendelea kupiga hatua kubwa kutokana na mabondia wake kutambulika au kutambuliwa na mashirikisho makubwa ya mikanda ya kimataifa ambayo mabondia wakubwa wamekuwa wakipigania mara kwa mara.
IBO ni Shirika la kimataifa la mchezo wa ngumi ambalo ni miongoni mwa mashirika manne yanayounda ‘Big Four’ ya mikanda mikubwa duniani ambayo kwa mara ya kwanza imewajumuisha mabondia tisa wa Tanzania katika orodha ya ubora wa viwango ‘Pound For Pound’ ya mabondia 100 bora wa kutoka katika kila uzani au kilo ambazo ngumi za kulipwa imekuwa ikatumbua makundi 17 ya kilo rasmi zinazopiganiwa.
Hii imekuwa ni mara ya kwanza kupitia mfumo rasmi wa IBO kuwatambua kwa kuwajumisha mabondia wengi wa Tanzania ambao tafsiri yake kuwa mchezo huo umepiga hatua kubwa katika daraja la kimataifa huku ukiwa umetoka katika migogoro ya kiuongozi kwa kipindi kirefu kabla ya serikali kuingilia kati kuweka sawa.
Makala haya inakuchambulia mabondia hao ambao wametajwa kwenye orodha hiyo.
Salmin Kassimu
Kwa sasa ndiye bondia namba moja nchini kwa mujibu wa Pound For Pound ya mabondia wote wa Tanzania na namba mbili Afrika lakini kwenye orodha ya IBO ametajwa katika nafasi ya 20 katika mabondia 100 bora duniani wa uzani wa Super Bantam wanatambulika na IBO akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 12 akiwa ameshinda kumi na mawili akitoka sare.
Mchanja Yohana
IBO wamelitaja jina la Mtanzania, Mchanja Yohana katika nafasi ya 22 katika mabondia 100 bora duniani katika uzani wa fly ndiyo Mtanzania aliyekamata nafasi ya pili katika mabondia waliotajwa katika viwango hivyo kutoka Tanzania.
Hassan Mwakinyo
Jina la bondia Hassan Mwakinyo kutoka katika udhani wa middle ametajwa kwenye nafasi ya 30 katika mabondia 100 bora duniani wa uzani huo ambao wametajwa kwenye nafasi ya viwango hivyo.
Mwakinyo ashika namba moja nchini kwenye uzani wake na Afrika lakini katika orodha ya IBO ambayo ameingia kwa mara ya kwanza baada ya kuwa kukaa kwa kipindi cha mwaka mmoja bila ya kupigana kabla ya kurejea ulingoni Disemba 26, mwaka jana.
Ibrahim Mafia
Ibrahim Mafia ametajwa katika nafasi ya 40 katika mabondia 100 bora wa uzani wa Bantam wanatambulika na IBO ambayo hii inamfanya kuwa ni miongoni mwa mabondia ambao wanaweza kuwania mikanda ya tasisi hiyo.
Richard Mtangi
Katika uzani wa middle kutoka Tanzania, IBO imemtaja Mtanzania mwengine ambaye ni bondia Richard Mtangi akiwa katika nafasi ya 48 katika mabondia 100 bora duniani baada ya Hassan Mwakinyo aliyetajwa kwenye nafasi ya 30.
Frank Shagembe
Kutoka katika uzani wa Light Heavy, ametajwa kijana wa kutoka katika jiji la Mbeya ambaye kabla ya kuwa bondia aliwahi kufanya kazi ya kuchimba madini katika migodi ya dhahabu Chunya, Frank Shagembe ambaye ametajwa katika nafasi ya 49 katika mabondia wa 100 bora wa uzani kwa mujibu wa orodha ya IBO.
Ibrahim Class
Mtaalam wa kupiga ngumi ya jabu Mtanzania, Ibrahim Class ni miongoni mwa mabondia ambao wametajwa kutoka kwenye orodha ya IBO inayojumuisha mabondia 100 bora akiwa kwenye nafasi ya 52 kutoka katika uzani wa super feather.
Mubarack Denso
Uzani wa fly umefanikiwa kuingiza mabondia 100 bora duniani wa IBO baada ya Mchanja Yohana, Mtanzania mwengine aliyeingia ni Mubarack Denso akiwa kwenye nafasi ya 80 katika mabondia 100 wa uzani huo.
Kalolo Amiri
Kalolo Amiri ni miongoni mwa mabondia waliotajwa kwenye orodha hiyo akitokea katika uzani wa bantam akiwa ni Mtanzania wa pili kutokea katika uzani huo baada ya Ibrahim Mafia, Kalolo anakamata nafasi ya 84 katika mabondia 100 bora duniani kwa mujibu wa IBO.