Ulaya. Baada ya kufanikisha  kuwa bondia maarufu duniani, safari ya pili kwa Jake Paul (29), ni kuanzisha uhusiano na Jutta Leerdam (27), mchumba wake wa sasa anayetuonyesha upande wa pili wa bondia huyo. 

Jake aliyejizolea umaarufu mkubwa kama mtengeneza maudhui mtandaoni (YouTuber) kabla ya kuhamia kwenye ndondi za kulipwa, uhusiano wake na Jutta umekutanisha ndoto za watu wanaotaka kuacha alama katika michezo.

Safari ya uhusiano wao imekuwa wazi sana kupitia mitandao ya kijamii lakini nyuma yake kuna hadithi ya watu wawili waliokutana, wakaelewana na kisha wakaamua kusimama pamoja katika nyakati zote za maisha.

Kwa mara ya kwanza wawili hao waliweka wazi uhusiano wao kwenye Instagram hapo Aprili 2023, na tangu wakati huo wamekuwa wakionyesha safari yao ya mapenzi ilivyo kupitia mitandao ambapo wana mamilioni ya wafuasi.

“Nakupenda sana, ninashukuru kuwa na wewe, unanifanya kuwa msichana mwenye furaha zaidi duniani. Mwanaume mwenye moyo wa kipekee zaidi,” aliandika Jutta kwenye Instagram Aprili 2024, kuadhimisha mwaka mmoja wa uhusiano wao.

Akizungumza kwenye podcast ya mpenzi wake, BS w/ Jake Paul Aprili 2023, Jutta alisema Jake ni mtu wa tofauti na anavyoonekana mtandaoni, huku Jake naye akieleza ya kwake.

“Si mjinga kabisa kwenye maisha halisi. Ni tofauti tu anapokuwa mbele ya kamera. Wewe ni mtu mzuri sana na nataka siku moja nikuonyeshe kwa watu ulivyo,” alisema na kuongeza.

“Tabia yako ya kwenye video unazoposti mtandaoni ni tofauti kabisa na ukilinganisha na ulivyo sehemu nyingine,” Jutta alimwambia Jake.

Jake alijibu akisema, “mbona nahisi niko vilevile”. Hata hivyo, Jutta alimkatisha mara moja akisema, “hapana, hapana, sivyo kabisa. Kwa kweli wewe ni mtulivu zaidi ukiwa kwenye maisha halisi. Umetulia zaidi”.

“Una upole wa dhati na unaonyesha hisia zako kwa uwazi. Sijawahi kuona mwanaume wa aina hiyo. Ni jambo la kiume sana kuweza kuonyesha hisia zako, na nafikiri hilo ni jambo zuri sana,” alisema Jutta.

Lakini, Jutta ni nani hasa? Mrembo huyo aliyezaliwa Desemba 30, 1998 huko ‘s-Gravenzande nchini Uholanzi, amejizolea umaarufu kupitia mchezo wa kuteleza kwenye barafu (speed skating) akishinda mataji kadhaa. 

Speed skating ni mchezo wa kuteleza juu ya barafu kwa kasi, ambapo wanamichezo hushindana katika umbali tofauti kama mita 500, 1000, 1500, 5000 au zaidi.

Hutumia viatu maalumu kushindana kukimbia kwa kasi kwenye uwanja wa barafu, na ni miongoni mwa michezo mikuu kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi.

Jutta aliuambia mtandao wa Infrostada Sports kuwa alianza kujihusisha na mchezo huo tangu akiwa na umri wa miaka 11, na hadi wakati huu umeendelea kumvutia.

Amejikita zaidi kwenye mashindano ya mbio fupi (sprint) na anashikilia rekodi kwenye mita 1,000. Alishinda taji lake la kwanza kubwa kwenye mashindano ya dunia ya vijana (World Junior Championships) 2017 nchini Finland.

Jutta aliiwakilisha Uholanzi kwenye Olimpiki mwaka 2022 iliyofanyika Beijing, China ambapo alijinyakulia medali ya fedha katika mbio za mita 1,000, akimfuatia Mjapani Takagi Miho aliyevunja rekodi upande wa wanawake.

“Hii ni Olimpiki yangu ya kwanza, nilikuwa nimelenga kushinda dhahabu, lakini nimefurahishwa pia na ushindi huu wa fedha,” alisema Jutta baada ya mashindano hayo.

Jutta ambaye kwa sasa anajiandaa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki 2026 itakayofanyika Milan nchini Italia, mbali na mchezo huu, yeye ni mtu mwenye ushawishi (influencer) mitandaoni akiwa na wafuasi milioni 5 Instagram.

Vilevile ni mwanamitindo, na mara nyingi kuposti Instagram picha za mitindo ya kisasa akitangaza chapa mbalimbali za mitindo na urembo kama Hugo Boss na Dior.

Siku zote Jutta amekuwa akimuunga mkono Jake katika kazi yake, mathalani alimpongeza mara baada ya kumshinda Mike Tyson katika raundi ya nne ya pambano kali lililorushwa na Netflix hapo Novemba 2024.

“Umecheza mchezo huu kwa miaka michache tu lakini tayari umeweza kuandaa matukio makubwa sana. Watu wanaweza kusema chochote, lakini wanakutazama na unaweka rekodi,” alieleza.

“Unaendelea kunionyesha mimi na dunia kwamba kuota ndoto kubwa na kuziamini kunafanya kazi. Jake Paul, ninajivunia sana juhudi zako,” aliandika Jutta kupitia Instagram baada ya pambano hilo. 

Kufikia Machi 21, 2025, bondia huyo akapiga goti moja chini akiwa amezungukwa na maua meupe na mishumaa, kisha akamvisha Jutta pete kubwa ya almasi, na huo ukawa mwanzo wa uchumba wao. 

“Tuna shauku kubwa ya kutumia maisha yetu yote pamoja,” Jake aliandika kwenye Instagram akiambatanisha na picha za tukio hilo.

Baadaye Jutta alizungumza na Jarida la People kuhusu hatua hiyo kubwa katika maisha yao na kusema kwake Jake ndiye mwanaume mwenye mapenzi ya kweli zaidi duniani, hivyo ana bahati sana kuwa naye!.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *