Kauli yake ni kwamba “Kukata tamaa sio chaguo watu wengi wanakutegemea wewe.” Mpango huo unalenga kutoa msaada wa kiteknolojia na elimu kwa wakulima wadogo ili kuimarisha mnepo katika kilimo.

Nchini Kenya, kilimo kinatoa ajira kwa takriban asilimia 75 ya idadi ya watu wa tafa hilo, lakini maisha ya wakulima yameanza kuwa hatarini kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa ardhi yenye tija, jambo linaloathiri bara zima la Afrika.

Kadri ukame na hali mbaya za hewa zinavyoongezeka nchini humo, Maryanne Gichanga anaamini ubunifu ni muhimu kusaidia jamii ya wakulima wa Kenya kujenga mnepo.

Akizungumza na Umoja wa Mataifa kabla ya Siku ya Kimataifa ya Nishati Safi, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Januari, anaelezea jinsi katika sekta inayotawaliwa na wanaume, amefaulu kuwapatia wakulima maarifa kuhusu afya ya udongo na miche pamoja na mifumo ya hali ya hewa kwa kutumia sensa zinazotumia nishati jua na data za satelaiti za akili mnemba (AI).

Kutoka kuwa mkulima hadi kusaidia wakulima

“Nililelewa katika familia ya wakulima. Wazazi wangu ni wakulima. Nilishuhudia mavuno mengi, lakini pale mabadiliko ya tabianchi yalipoanza, hatukuelewa kilichokuwa kinaendelea. Kwa kuwa kilimo kilikuwa chanzo chetu cha kipato, mavuno mabaya yaliathiri moja kwa moja maisha yetu na hata kushindwa kwenda shule.” amesema Maryanne

Maryanne anaongeza kuwa  siku zote alitaka kutoa suluhu kwa wazazi wake na familia nyingine za wakulima. Hii ndiyo iliyomchochea kuanzisha kampuni yake na kuungana na watu wenye mawazo sawa kujenga suluhu hii kusaidia wakulima wadogo.

Greenovations Africa ni mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa unaosaidia wanawake wajasiriamali kama Maryanne, umekuwa sehemu muhimu ya mchakato, kwa kuwa walikuwa na imani na kampuni ndogo, na walitoa mafunzo pamoja na mtaji wa kuanzia  ili kusaidia ukuaji wao.

Maryanne Gichanga, mjasiriamali wa kilimo wa Kenya, amesimama kando ya sensor ya IoT katika uwanja wa mboga mboga, akionyesha suluhisho zake za kilimo zinazotokana na teknolojia.

© Agritech Analytics

Wakulima nchini Kenya wanatumia zana mpya za data ili kuboresha tija katika kilimo chao.

Kukata tamaa sio chaguo

“Afrika, jamii nyingi ni za kike zinaongozwa na wanaume . Kuingia katika sekta inayotawaliwa na wanaume ni changamoto. Watu wangependelea kufanya kazi na mwanaume, wakidhani wanaume wanaelewa kilicho kwenye kazi yangu kuliko mimi. Katika sehemu nyingi, hawaamini uongozi wa wanawake, hata wanawake kutoa suluhu si jambo linalopokelewa kwa urahisi.”  amesema Maryanne.

Maryanne kaendelea kusisitiza kuwa kilichothibitisha ajabu katika safari hii ni uvumilivu, pamoja na mafunzo na maonesho kuonesha kile wanachofanya na kwamba wanajua wanachokifanya.

Anasema huwezi kukata tamaa unaposhirikiana na watu unaokutana nao na hatimaye utafanikiwa “Ni muhimu kukumbuka sababu ya kuanza, kujua wazazi wangu hawana tena shida, na kufikiria mamilioni ya watoto walio na wazazi wakulima, na mustakabali wa watoto hao ungekuwa hatarini iwapo wazazi wao hawatapata kipato thabiti. Wakati mwingine ukitazama urefu wa safari yako, unajua kukata tamaa sio chaguo. Watu wengi wanakutegemea wewe, na hilo ndilo linanifanya nishikilie lengo langu.” Ameongeza

Faraja yake

Maryanne anasema hufurahia zaidi pale anapoona maisha ya watu yakibadilika moja kwa moja, akieleza kuwa kuwawezesha wakulima hubadili maisha yao. 

Amesisitiza kuwa kuona mavuno yakiongezeka au watu wakiondokana na changamoto huwapa motisha ya kufanya kazi kwa bidii zaidi

Kwa mujibu wake, kuona mkulima ambaye hapo awali hakuwa na uwezo wa kununua mbegu sasa akiwa na udhibiti wa bei ya mavuno yake ni faraja na kichocheo kikubwa kwake.

Wito kwa wengine

Maryanne anawahimiza wanawake na wasichana wengine wanaotaka kuanzisha ubunifu katika kilimo au hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kujaribu bila woga, akisema kwamba watapata kujifunza njiani na kwamba kuna watu wengi walio tayari kutoa msaada wa kifedha, wa kiufundi, ushauri na mafunzo. 

Ameongeza kuwa hakuna wakati muafaka au sahihi wa kuanza na kwamba mtu hawezi kuwa tayari kikamilifu, bali kinachohitajika ni kuanza bila kuogopa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *