
Tukio hilo linajiri baada ya mamlaka za Israel “kuvamia na kubomoa majengo yaliyoko katika eneo hilo wiki iliyopita”, kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini.
“Kuruhusu uharibifu huu ambao haujawahi kushuhudiwa ni shambulio la karibuni zaidi dhidi ya Umoja wa Mataifa katika juhudi zinazoendelea za kubomoa hadhi ya Wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kimabavu na kufuta historia yao,” amesema Bwana. Lazzarini.
Katika taarifa fupi, afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa “hakuna mipaka kwa dharau dhidi ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kimabavu”.
Ukiukwaji wa sheria za kimataifa
Hatua ya mamlaka za Israel Jumanne iliyopita ya kupeleka tingatinga katika eneo la Sheikh Jarrah, ambako zilivunja majengo ya UNRWA, ilizua lawama na shutuma za haraka kutoka kwa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa akiwemo Katibu Mkuu António Guterres na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk.
Kabla ya tukio hilo kubwa, tarehe 14 Januari, vikosi vya Israel viliingia katika kituo cha afya cha UNRWA huko Yerusalem Mashariki na kuamuru kifungwe. Shirika hilo liliripoti kuwa wafanyakazi wake walikuwa “na hofu kubwa na kwamba hali inayozidi kuzorota ni matokeo ya moja kwa moja ya sheria zilizopitishwa na bunge la Israel mwezi Desemba, zilizoongeza nguvu kwa sheria zilizopo dhidi ya UNRWA zilizopitishwa mwaka 2024.”
Majengo ya UNRWA pia yamelengwa na wachomaji moto katikati ya kile Kamishna Mkuu wa shirika hilo amekiita “kampeni kubwa ya upotoshaji wa taarifa dhidi ya UNRWA inayoendeshwa na Israel”.
Haya yote yametokea licha ya uamuzi wa mwezi Oktoba uliopita wa mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), uliosisitiza kuwa Israel ina wajibu wa “kuwezesha shughuli za UNRWA, si kuzizuia au kuzipinga.”
Bwana. Lazzarini amesema mahakama hiyo pia ilisisitiza kuwa Israel haina mamlaka juu ya Yerusalem Mashariki.