Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Oscar John Lelo anayefahamika kisanii kama Whozu ni mmoja wa wanamuziki waliopitia safari ya kipekee na kuvutia kabla ya kufikia mafanikio aliyonayo wakati huu akisimama kama chapa yenye ushawishi.
Whozu, mkali wa kibao cha Ameyatimba (2023), yeye ni msanii, mtunzi wa nyimbo na mburudishaji mwenye uwezo mkubwa wa kuchanganya sanaa ya ucheshi na muziki kwa namna inayowavutia mashabiki wengi.
Kwa wanaomfuatilia unatambua kuwa muziki wa Whozu una ladha ya kipekee, ukiwa na mchanganyiko wa Pop, RnB, Afrobeat na sauti za asili za Kaskazini mwa Tanzania ambapo ndipo amezaliwa na kukulia.
Alianza kufanya muziki akiwa Chuo cha Ushirika Moshi, baadaye alipohamia Dar es Salaam akaanza kuzifukuzia ndoto zake za muda mrefu. Hata hivyo, mafanikio yake hayakuja kwa njia ya kawaida kwa kuwa safari yake ilianza kama utani tu, pale alipokuwa akichanganya muziki na vichekesho kupitia mitandao ya kijamii hasa Instagram. Wengi hawakumchukulia kwa uzito mwanzoni lakini ghafla jina lake likaanza kuchukua nafasi kubwa ndani ya Bongofleva, huku akiwa na ukaribu na baadhi ya mastaa wenye majina makubwa katika muziki huo.
Alipata msaada kutoka kwa rapa wa kundi la Weusi, Nikki wa Pili ambaye alikuwa mshauri wake wa karibu, akimuelekeza njia sahihi ya kupita katika muziki, hata kumchagulia wasanii wa kuwasikiliza ili kujifunza.
Baada ya kupambana kwa muda mrefu bila kuona mafanikio makubwa, Whozu alibadili mkakati. Aligeukia uchekeshaji kupitia muziki kwa kuanza kurudia nyimbo za wasanii maarufu kwa mtindo wa vichekesho. Na hii ndio iligeuka kuwa mlango wake wa mafanikio, video zake zilianza kusambaa kwa kasi mitandaoni, zikimpa umaarufu mkubwa na kumfanya ajulikane zaidi kama mburudishaji mwenye kipaji cha kipekee.
Umaarufu wake ulipanda kwa kasi zaidi pale Diamond Platnumz alipoposti Instagram video yake akicheza kwa mtindo wa kuchekesha wimbo Rockonolo (2017), alioshirikisha na Lumino, Mohombi na Franko.
Wakati huo Whozu alikuwa na wafuasi takribani 5,000 tu Instagram, lakini ndani ya muda mfupi akafikisha 10,000 kutokana na nguvu ya Diamond katika mtandao huo.
Leo hii, Whozu ana wafuasi milioni nne, na huu ni uthibitisho kuwa jina lake linatambulika na wengi, na tayari ana nguvu ya ushawishi katika kile anachokifanya.
Wakati akiendelea kujitafuta, Whozu alipata nafasi ya kuonekana kwenye video ya wimbo wa kundi la Weusi, Nicome (2017) ambayo ndani yake ilikuwa na wasanii wengi maarufu. Hii ni sawa na namna Mimi Mars alivyowahi kuonekana kwenye video ya wimbo wa kundi la Navy Kenzo, Game (2015), kabla hajaanza muziki wake, hivyo haya yalikuwa ni maandalizi ya safari kubwa.
Katika harakati za kutafuta mafanikio, Whozu alikutana na wasanii wengine waliokuwa wanapambana kutoka kwa wakati huo, baadhi ya wasanii hao ni Marioo, Kusah na kundi la Mabantu.
Urafiki na ushirikiano wao uliwasaidia wote kufanikisha lengo lao kuu, na hadi leo wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao za muziki wakitengeneza nyimbo ambazo zimepokelewa vizuri.
Kati ya nyimbo hizo ni Vavayo (2023), wake Whozu akimshirikisha Marioo. Wimbo huu wenye ladha ya Amapiano ulitamba kwa muda mrefu na hadi sasa video yake imetazamwa YouTube mara milioni 3.5.
Mwaka 2018, Whozu aliachia wimbo ‘Huendi Mbinguni’ uliokuwa na vituko vingi na ujumbe wa kuchekesha lakini wenye kugusa jamii ukitoa ujumbe muhimu kuhusu maisha.
Ukiwa umetayarishwa na S2kizzy, wimbo huu ulimtangaza zaidi Whozu na kumpatia mafanikio makubwa ya kifedha kwa mara kwanza hadi kuweza kununua gari lake la kwanza aina ya Crown.
Kwa sehemu kubwa mafanikio hayo yalitokana na wimbo huo kutumika kama wimbo rasmi wa tamasha la Fiesta 2018, hatua iliyomuweka Whozu kwenye ramani ya wasanii wakubwa Tanzania.
Na kipindi cha Fiesta 2018 mkoani Dodoma, ndipo Whozu alikutana na Tunda ambaye walikuja kuanzisha uhusiano uliogusa hadi muziki wake. Hata hivyo, walikuwa wakifahamiana tangu wanasoma Moshi, basi Tunda akaja kutokea katika video ya wimbo wa Whozu, Doko (2019), kabla ya kuachana. Lakini wameendelea kuwa na ukaribu kwa sababu ya mtoto wao.
Wakati muziki wa amapiano kutokea Afrika Kusini unaanza kushika kasi Bongo, Whozu alikuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzo kuimba mahadhi hayo na kupokelewa vizuri.
Whozu amefanya vizuri zaidi na nyimbo za Amapiano kama Sijui Nikoje (2022), Vavayo (2023) na Ameyatimba (2023) ambao remix yake aliwashirikisha Billnass na Mbosso.
Miaka yake minane ya umaarufu katika muziki, Whozu amefanikiwa kushirikiana na wasanii wengine kama Baddest 47, Zuchu, Ibraah, Gigy Money, D Voice, Rayvanny, Hamadai, Alikiba na kadhalika.
Kwa upande wa maisha binafsi, Whozu ana uhusiano na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, staa wa filamu ambaye ameshinda tuzo kama Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF), Hollywood And African Prestigious Awards (HAPAWARDS) na kadhalika.