Dar es Salaam. Katika kuelekea mabadiliko makubwa ya kimaendeleo nchini hasa wakati huu wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, mjadala kuhusu ubora wa elimu yetu na mchango wake katika kuliendelezaTaifa unazidi kupamba moto.

Mwandishi wetu amefanya mahojiano ya kina na Profesa George Kuhangwa, ambaye ni Mkuu wa idara ya misingi ya elimu, menejimenti na uendelevu katika Shule Kuu ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 

Katika mahojiano haya, Profesa Kuhangwa anachambua kwa kina mfumo wa elimu nchini, akiangazia   mitalaa mipya, changamoto ya ugharamiaji wa elimu na hadhi ya mwalimu nchini na masuala mengine muhimu ya kielimu.

​Swali: Je, mfumo wa elimu wa sasa unamjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa mtatuzi wa changamoto za kijamii, au bado tunazalisha wahifadhi wa nadharia?

​Jibu: Kwa kiasi kikubwa, mfumo wetu bado umeegemea kwenye ‘kalamu na karatasi’. Hata hivyo, maisha ya uhalisia hayahitaji karatasi kila wakati. 

Katika ujenzi wa maarifa, kuna nyanja tatu: utendaji, akili, na hisia. Kwa sasa, shinikizo kubwa liko kwenye uwezo wa akili pekee, tena kwa lengo la kufaulu mitihani. Tunapaswa kuhama kutoka kwenye kuangalia mwanafunzi amefaulu vipi, na badala yake tuangalie amejifunza nini na anaweza kufanya nini kwa vitendo.

​Swali: Serikali inatekeleza mpango wa elimu bila ada. Tunawezaje kuhakikisha wingi wa wanafunzi hauathiri ubora wa kile wanachojifunza?

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa George Kahangwa.

​Jibu:  Ni lazima tutambue gharama halisi ya kutoa elimu bora. Elimu bora ina gharama, na ni lazima nchi ifanye tathmini ya kina kuhusu kiasi kinachohitajika kumwandaa mtoto mmoja katika mazingira ya sasa. Bajeti ya elimu lazima iendane na mahitaji halisi. Elimu bila ada isiwe ‘bora liende’; hili lisiachwe kwa Serikali pekee, bali wadau wote washiriki kwa mustakabali wa rasilimali watu ya Taifa.

​Swali:  Ni kwa kiwango gani mitalaa ya sasa inaendana na mahitaji ya soko la ajira, sayansi, teknolojia na uchumi wa viwanda ambao Tanzania inalenga?

​Jibu: Maboresho ya mitalaa ni mazuri na yanazingatia mahitaji ya soko, lakini changamoto kubwa iko kwenye utekelezaji. Kwa mfano, mtalaa mpya umekuja na elimu ya amali, huwezi kutoa elimu ya amali  bila vifaa wala walimu waliobobea. Huwezi kufundisha somo la kompyuta kwa kuchora ubaoni. Bila uwekezaji mkubwa wa fedha kwenye vifaa, mitalaa hii itabaki kuwa nadharia. Tukiamua kuweka kipaumbele, uwekezaji huu unawezekana.

​Swali: Kuna uhaba mkubwa wa walimu wa sayansi na hisabati. Ni mbinu gani za kimkakati zinaweza kutumika kuziba pengo hili?

​JIbu: Hili ni suala la kimkakati zaidi. Kwanza, tunapaswa kuwatumia walimu wachache tulionao ‘kuzalisha’ wengine wengi. Pili, Serikali inaweza kuiga mifano ya shule binafsi kwa kuwawahi vijana wanaohitimu masomo ya sayansi vyuoni na kuwapa motisha ya kufundisha.

​Pia, tunaweza kutumia teknolojia kuruhusu wanafunzi kujifunza hata pasipo na mwalimu wa moja kwa moja. Vilevile, kuwepo na ‘ujirani mwema’ ambapo shule binafsi zenye ziada ya walimu wa sayansi zinashirikiana na shule za umma zilizopo kwenye kata moja. Yote haya lazima yaende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya walimu ili kuwavutia vijana kubaki kwenye taaluma hii.

​Swali: Kumekuwa na mvutano wa muda mrefu kuhusu lugha ya kufundishia kati ya Kiswahili na Kiingereza. Nini mwelekeo sahihi kwa Tanzania?

​Jibu: Ni rahisi kwa mwanafunzi kuelewa kupitia lugha anayoijua vyema. Hata hivyo, ushauri wangu ni kuzifundisha lugha hizi kama lugha kwanza kabla ya kuzifanya kuwa lugha za kufundishia. Kama ni Kiswahili, kifundishwe kwa umahiri. Kama ni Kiingereza, tunaweza kuwa na programu za kubadilishana wataalamu, hata kuleta walimu kutoka Uingereza kwenye vyuo vyetu vya ualimu. Ukweli ni kwamba hatuwezi kuikwepa lugha ya Kiingereza katika mawasiliano ya kimataifa, hivyo lazima tujipange vyema kuitawala.

​Swali: Je, kuna mgongano wowote kati ya elimu ya amali inayotolewa sekondari na ufundi stadi unaotolewa na mamlaka kama VETA?

​Jibu: Sioni mgongano, bali uwezekano wa kukamilishana. Uhitaji wa elimu ya ufundi ni mpana sana. Katika kipindi hiki chenye changamoto ya ajira, tunahitaji taasisi nyingi zaidi zinazotoa maarifa ya kujiajiri. Hata kama sekondari zote zitatoa elimu ya amali, bado tutahitaji vyuo vya ufundi kwa ngazi za juu za utaalamu.

​Swali: Jamii bado inaona elimu ya ufundi ni kwa ajili ya ‘waliofeli’. Tunabadilishaje mtazamo huu?

​Jibu: Huu ni mtazamo wa kikoloni uliodumu kwa miaka mingi. Ili kuubadili, tunahitaji mkakati wa vitendo. Mkondo wa amali usichukue wanafunzi wenye alama za chini pekee; tuwe na wanafunzi wenye ufaulu wa juu wanaoingia kwenye ufundi kwa hiari na mapenzi. Pia, hadhi na fursa za ajira kwa wahitimu wa amali lazima zilingane na zile za mkondo wa kawaida ili kuondoa ubaguzi wa kitaaluma.

​Swali: Je, mfumo wetu wa upimaji na mitihani unajenga uelewa au unahimiza ushindani wa alama tu?

​Jibu: Ukweli ni kwamba bado hatujafanya ‘upimaji’ wa kweli; tunafanya mitihani ya karatasi. Kupima kunatakiwa kubaini mwanafunzi anaweza kufanya nini. Kama amejifunza upasuaji wa viumbe, upimaji uwe ni yeye kufanya upasuaji huo kwa vitendo. Pia, tunahitaji ugatuzi wa madaraka ya upimaji; kazi hii ianzie ngazi ya shule na wilaya badala ya kutegemea mtihani mmoja wa kitaifa ambao hauwezi kuibua vipaji vya kila mtoto.

​Swali: Katika zama hizi za mmomonyoko wa maadili, elimu yetu inatimiza wajibu wake wa kujenga uzalendo na uadilifu?

​Jibu: Tuna masomo ya historia na maadili, lakini tatizo ni mazingira ya jamii. Mwanafunzi anaweza kupata daraja ‘A’ la maadili darasani, lakini akitoka nje anakutana na jamii inayowaenzi wasio waadilifu. Tunashuhudia ‘machawa’ au watu wanaotumia ujanja ujanja wakifanikiwa kuliko wasomi. Hii inakinzana na kile tunachofundisha. Ili elimu ijenge uzalendo, ni lazima mfumo wa jamii uonyeshe kuwa uadilifu unalipa.

​Swali: Teknolojia ya Akili Unde (AI) ni fursa au tishio kwa elimu yetu?

​Jibu: AI ni teknolojia ambayo hatuwezi kuikwepa, hivyo ni lazima tuikumbatie kwa nidhamu. Ni fursa kubwa ya kutafuta maarifa na kubuni ajira. Hata hivyo, kuna hatari ya wanafunzi kuacha kutumia akili zao. Tunahitaji sera na miongozo itakayoelekeza namna ya kuitumia kama nyenzo ya utafiti na sio mbadala wa fikra za mwanafunzi. Pia, lazima tufundishe watu wetu kutofautisha kati ya maudhui halisi na yale yaliyotengenezwa na mashine.

​Swali: Mageuzi gani makubwa unatamani kuyaona katika miaka 10 ijayo ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi?

​Jibu: Kwanza, kuwianisha ubora wa elimu kati ya shule za umma na binafsi ili kuzuia matabaka. Pili, kuongeza uwekezaji kwenye tafiti katika elimu ya juu. Tatu, kufanya mapitio ya kila kinachofundishwa ili kiwe na maana kwa maisha ya sasa. Lakini kubwa zaidi kuliko yote, ni kurejesha hadhi ya mwalimu. Tukiendelea kuwa na mwalimu mwenye hali mbaya ya kimaisha, tutakuwa na elimu inayofanana na hali yake. Lazima tuchore upya wasifu wa mwalimu anayestahili kuandaa Taifa la kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *