
Kampuni ya kusafirisha mizigo ya United Parcel Service (UPS) ya Marekani imetangaza kwamba, itawatimua kazi watu 30,000 zaidi mwaka huu, katika juhudi za kupunguza ushirikiano wake na shirika la Amazon, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango wake wa ‘uokoaji’ na kubana matumizi.
Afisa Msimamizi wa Fedha wa UPS, Brian Dykes amewaambia wawekezaji kwamba, kampuni hiyo inakusudia kupunguza saa za kazi ili ‘kuokoa’ dola milioni 25, kutokana na kupungua kwa miamala na shirika la Amazon.
“Kwa upande wa gharama zinazobadilika, tunatarajia kupunguza nafasi takriban 30,000 za kazi,” Dykes amesema na kuongeza kuwa, “Hili litatimizwa kupitia kufutwa kwa huduma, na tunatarajia kutoa mpango wa pili wa kuachisha kazi kwa hiari madereva wenye mikataba.” Zaidi ya hayo, UPS imesema vituo vyake 24 vitafungwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2026, na vingine zaidi yumkini vitafungwa baadaye mwaka huu.
Kupungua ukuaji wa uchumi na kuongezeka mfumuko wa bei huko Marekani pamoja na kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo yameilazimisha kuamua kuachisha kazi idadi kubwa ya wafanyakazi wake.
Hivi karibuni pia, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Amazon la Marekani alisema kuwa kampuni hiyo imewafuta kazi wafanyakazi zaidi ya 18,000. Baadhi ya waajiri wakubwa wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Walmart, Facebook na Pepsi, hivi karibuni wamepunguza maelfu ya nafasi za kazi nchini humo kutokana na mdororo wa uchumi.