Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Uganda (UPDF), , amezua mjadala mkubwa baada ya kuutuhumu ubalozi wa Marekani nchini humo kwa kumficha kiongozi wa upinzani Bobi Wine.

Jenerali Kainerugaba ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni amezusha mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha mfululizo wa jumbe akilaumu Ubalozi wa Marekani nchini Uganda kwamba, umemficha kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine.

Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni katika oparesheni maalumu za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda ulihusika kusaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026. Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi alisema:

“Wananchi wenzangu wa Uganda, kutokana na hali ya sasa ambapo kiongozi wa upinzani amejiteka mwenyewe na kutoweka, na kwa mujibu wa taarifa zetu bora za kijasusi, vitendo hivi vilifanyika kwa ushirikiano na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini mwetu. Kwa sababu hiyo, UPDF imesitisha ushirikiano wote na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani jijini Kampala. Hii inajumuisha pia ushirikiano wetu nchini Somalia. Ushirikiano wa kiusalama uliokuwa wa thamani kubwa kati ya Uganda na Marekani umeathiriwa vibaya tangu mwaka 2015 na watendaji wa urasimu wasio na ubunifu katika ubalozi huo.”

Hata hivyo baadaye, Jenerali Muhoozi alifuta ujumbe huo na kumuomba radhi kwa kauli zake.

Aidha, alionya kuwa nguvu yoyote ya kigeni itakayojaribu kumtorosha Kyagulanyi nje ya nchi italeta mgawanyiko mkubwa wa kidiplomasia kati ya Uganda na mataifa husika.

Tukio hilo limezidi kuchochea mvutano wa kisiasa na kidiplomasia nchini Uganda, huku likizua maswali mapya kuhusu haki za kiraia, usalama na nafasi ya wahusika wa kimataifa katika siasa za ndani za taifa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *