Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mhe. Khalid Nsekela, amempongeza Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah Ulega kwa hatua ya serikali kuanza utekelezaji wa mradi wa barabara ya Omurushaka–Karagwe hadi Rwenkorongo (Kyerwa), akisema ni uthibitisho kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ni serikali sikivu inayojali mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na Wananchi wa Jimbo La Kyerwa waliojitokeza Kumsikiliza Waziri wa Ujenzi Mhe. Nsekela amesema barabara hiyo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Kyerwa kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.

“Barabara hii ilikuwa imekwama kwa muda mrefu na imekuwa kilio kikubwa cha wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Niliwasilisha ombi hili bungeni nikitambua mateso ambayo wananchi wangu wamekuwa wakiyapitia, hivyo napenda kumpongeza Waziri wa Ujenzi kwa kusikiliza na kuchukua hatua,” alisema Mhe. Nsekela.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua changamoto za wananchi, hususan waishio maeneo ya pembezoni.

“Hii ni ishara tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni serikali sikivu, inayosikiliza na kutekeleza kwa vitendo,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo aliwapongeza wananchi wa Jimbo la Kyerwa kwa kuendelea kumuamini yeye pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema imani hiyo imekuwa chachu ya yeye kuendelea kupigania maendeleo yao bungeni.

“Nawapongeza sana wananchi wa Kyerwa kwa kuendelea kuniunga mkono na kuendelea kukiamini CCM. Imani yenu ndiyo nguvu yangu ya kuendelea kupigania miradi ya maendeleo kama hii,” alisema.
Mhe. Nsekela aliahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *