Taarifa ya UNHCR iliyotolewa Jumanne Februari 24, huko Geneva, Uswisi, zaidi ya wakimbizi 90,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamekimbilia Burundi katika miezi mitatu iliyopita.

“Wengi wao wamehifadhiwa katika eneo ya wakimbizi ya Busuma, ambayo sasa inahifadhi zaidi ya raia wa DRC 66,000 waliowasili tangu mwishoni mwa mwaka 2025,” imesema taarifa hiyo.

Magonjwa na makazi ni changamoto

Akizungumza baada ya ziara rasmi nchini humo wiki iliyopita, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR anayeshughulikia Ulinzi wa Wakimbizi, Ruvendrini Menikdiwela, alielezea hali mbaya katika eneo hilo, akibainisha uhaba mkubwa wa maji safi, chakula, dawa, makazi na huduma za ulinzi. 

Kipindupindu na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika bado ni tishio kubwa, huku karibu watu 10,000 wakisalia katika vituo vya mpito vyenye miundombinu duni wakisubiri kuhamishiwa Busuma, ambayo tayari imeelemewa.

Ufadhili unasuasua wakati warundi wanarejea pia kutoka Tanzania

UNHCR imesema kuwa kati ya dola milioni 35 zinazohitajika mwaka huu kutoa msaada wa kuokoa maisha nchini Burundi, ni asilimia 20 pekee iliyopatikana hadi sasa. Kwa ujumla, Burundi inahifadhi zaidi ya wakimbizi 230,000, wengi wao kutoka DRC.

Shinikizo hilo linaongezeka huku pia kukiwa na wimbi la warundi wanaorejea kutoka uhamishoni, hasa kutoka Tanzania. Katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2026 pekee, zaidi ya warundi 28,000 wamerejea kutoka Tanzania, idadi inayozidi malengo ya makubaliano ya urejeaji wa hiari yaliyowekwa Novemba 2025 kati ya serikali husika na UNHCR.

Shirika hilo limeeleza wasiwasi wake kuhusu taarifa za ubomoaji wa makazi ya wakimbizi nchini Tanzania wakati wa urejeaji wa kasi wa hivi karibuni, hali iliyowalazimisha baadhi yao kuishi katika vituo vya kuondokea vilivyojaa kupita kiasi. 

Kambi ya Busuma ni ya dharura tuwekeze kwa jamii zinazowapokea

Kuhusu hali katika kambi ya Busuma, UNHCR inapendekeza hatua za haraka za kuongeza ufadhili ili kukidhi mahitaji ya msingi, kuimarisha huduma za maji na afya, na kuzuia milipuko ya magonjwa.

 Hata hivyo, shirika hilo linasema kuwa kambi za dharura kama Busuma ni suluhisho la muda mfupi tu.

Badala yake, linatoa wito kwa washirika wa kimataifa kuunga mkono mbinu za kuwahifadhi wakimbizi ndani ya jamii zinazowapokea, kwa kuwekeza katika huduma na miundombinu itakayowanufaisha wakimbizi na wananchi wa Burundi kwa pamoja.

UNHCR imesisitiza kuwa mshikamano wa kimataifa na ufadhili wa haraka na endelevu ni muhimu ili kuhakikisha wakimbizi wanalindwa na wale wanaorejea wanaweza kujumuika tena katika jamii zao kwa heshima na kujitegemea. “Bila hatua hizo, maisha ya maelfu ya watu yako hatarini,” imetamatisha taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *