Akirejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wa mazungumzo kati ya Kabul na Islamabad, mtaalamu huru wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Afghanistan, Richard Bennett, amesema mvutano unaoongezeka umezidisha hatari na changamoto kwa Waafghanistan wanaolazimika kurejea nchini kwao.

Mustakabali wa kutisha kwa wanaorejea

“Nilikuwa Pakistan hivi karibuni, nilizungumza na Waafghanistan huko ambao wana hofu kubwa kuhusu mustakabali wao,” amesema Bennett.

“Wanaamini kwamba kurejea Afghanistan hakutamaanisha tu maisha ya umaskini, bali kwa makundi fulani watetezi wa haki za binadamu, wanahabari, wanachama wa vikosi vya usalama na waliokuwa wanajeshi wa serikali iliyopita wako katika hatari dhahiri ya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa njia ya vurugu. Na tumeona ongezeko la matukio hayo katika miezi ya hivi karibuni.”

Mtaalam huyo maalum, ambaye hafanyi kazi moja kwa moja kwa Umoja wa Mataifa wala kulipwa kwa jukumu hilo, ametoa wito wa “busara na utulivu” wakati mvutano wa kikanda na kijiografia ukiendelea kupanda, akisisitiza matumaini kwamba “washirika wa tatu watasikilizwa” ili kupunguza hali hiyo.

Mapigano ya mpakani

Katika miaka ya hivi karibuni, Afghanistan imeshuhudia idadi kubwa ya raia wake inayokadiriwa kufikia milioni 2.7 mwaka 2025 wakirejea kutoka nchi jirani ikiwemo Pakistan.

Ndege za kijeshi za Pakistan zinaripotiwa kushambulia miji mikubwa ikiwemo Kabul na Kandahar usiku wa kuamkia leo Ijumaa.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan amesema nchi yake sasa iko katika “vita vya wazi” na Afghanistan, baada ya miezi kadhaa ya mapigano ya hapa na pale mpakani licha ya tangazo la kusitisha mapigano Oktoba mwaka jana.

Mzigo wa kibinadamu waongezeka

Bennett ameonya kuwa ongezeko hilo la mapigano litaongeza mateso kwa wananchi wa Afghanistan, akisisitiza hali mbaya ya kibinadamu inayokabili taifa hilo tangu Taliban warejee madarakani Agosti 2021.

Sekta ya afya ni moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na sera za mamlaka ya Taliban, ambazo zimekosolewa kimataifa kama mfumo wa ubaguzi wa kijinsia unaowaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake na wasichana.

“Katika maeneo mengi ya nchi, matibabu yametenganishwa kwa misingi ya kijinsia, hivyo wanawake wanapaswa kutibiwa na wanawake wenzao, na wanaume na wanaume,” ameeleza Bennett. “Kwa ujumla kuna upungufu wa wahudumu wa afya si madaktari pekee, tunazungumzia wakunga, wauguzi, mfumo mzima wa wahudumu wa afya.”

Ameongeza kuwa hata pale ambapo baadhi ya amri za Taliban hazitekelezwi kikamilifu, “sio tu kupata matibabu bali hata kufika kwenye huduma ndiko kuna changamoto, kutokana na vikwazo vikubwa vya uhuru wa kutembea.”

Mfumo wa afya wa Afghanistan tayari ulikuwa dhaifu kabla ya Taliban kutwaa Kabul baada ya miongo kadhaa ya vita, umaskini na uwekezaji mdogo. “Kuna hatari ya janga kamili la afya, hasa kwa wanawake na wasichana,” ameonya Bennett.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *