Katika kuendeleza dhamira yake ya kuwa karibu zaidi na wananchi na kusogeza huduma za bima karibu na jamii, kampuni ya Strategis Insurance Tanzania Limited imefungua rasmi kituo chake kipya cha mauzo jijini Mbeya.

Uzinduzi huo umefanyika katika hafla fupi iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha na bima, viongozi wa Serikali pamoja na wajasiriamali wa mkoa huo.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, ambaye aliipongeza Strategis kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika jiji hilo linalokua kwa kasi kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance (Kitengo cha Bima za Mali na Ajali), Jabir Kigoda, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa (kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance (Kitengo cha Bima za Mali na Ajali), Jabir Kigoda wakiwasili kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha mauzo la Strategis Insurance jijini Mbeya.

“Strategis tumejizatiti kuendelea kuwa jirani wa kweli katika kulinda ndoto, malengo na mipango ya watu wote. Kituo hiki si kwa ajili ya kampuni ya Strategis pekee, bali ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mbeya,” alisema Kigoda.

Kwa upande wake, Mhe. Malisa alieleza kuwa Mbeya ni miongoni mwa miji yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kutokana na sekta za kilimo, madini, biashara na usafirishaji.

“Mbeya ni jiji lenye nuru na ishara kubwa ya kukua. Limeendelea kuwa na fursa nyingi za kiuchumi, ikiwemo kilimo, madini na biashara. Strategis Insurance inapaswa kujipanga kuhakikisha inaleta bidhaa za bima zinazoendana na mahitaji mahususi ya soko hili,” alisisitiza Mhe. Malisa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance (Kitengo cha Bima za Mali na Ajali), Jabir Kigoda akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo kipya cha mauzo cha Strategis Insurance jijini Mbeya.

Ufunguzi wa kituo cha Mbeya ni sehemu ya mpango mpana wa Strategis wa kupanua wigo wa huduma zake nchini, sambamba na kuimarisha elimu ya bima kwa jamii. Kampuni hiyo inajivunia uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika soko la Tanzania, ikitoa masuluhisho mbalimbali ya bima yanayolenga kulinda maisha, mali na uwekezaji wa Watanzania.

Kupitia uwepo wake jijini Mbeya, Strategis inatarajia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ushirikiano na wadau wa biashara, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Kwa hatua hii, Strategis Insurance inaendelea kuthibitisha kauli yake ya kuwa mashirika wa maendeleo karibu na wananchi, karibu na ndoto zao, na karibu na mustakabali wa uchumi wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *