Dar es Salaam. Utafiti  umebaini kuwa zaidi ya nusu ya wagonjwa wanaoishi na kisukari, shinikizo la damu au magonjwa yote mawili nchini,  hawana uelewa wa kutosha kuhusu lishe inayofaa kwa afya zao. 

Wataalamu wanasema hali hiyo inaweza kudhoofisha juhudi za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza hatari ya kupata madhara makubwa ya kiafya.

Matokeo hayo yanatokana na utafiti uliopewa jina “Dietary Knowledge and Its Associated Factors Among Patients with Diabetes and Hypertension in Tertiary Hospitals in Dodoma, Tanzania: A Cross-sectional Study,” uliofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Utafiti ulihusisha wagonjwa 335 waliokuwa wamegundulika kuwa na kisukari, shinikizo la damu au magonjwa yote mawili kati ya Julai na Septemba mwaka 2021.

Washiriki walichaguliwa kwa njia ya nasibu, huku taarifa zikikusanywa kwa kutumia dodoso maalumu lililosimamiwa na watafiti.

Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa katika Jarida la East African Health Research, yanaonyesha kuwa asilimia 53.4 ya washiriki walikuwa na uelewa usiotosha kuhusu lishe bora inayopaswa kufuatwa katika kudhibiti magonjwa hayo.

Kati ya washiriki wote, asilimia 47.8 walikuwa na shinikizo la damu pekee, asilimia 21.2 walikuwa na kisukari pekee, huku asilimia 31 wakiwa na magonjwa yote mawili.

Uchambuzi wa utafiti umeonyesha kuwa watu wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 44, walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na uelewa mdogo kuhusu lishe ikilinganishwa na makundi mengine ya umri.

Aidha, watu wasiokuwa na ajira pamoja na wale waliokuwa wakitumia pombe, walibainika kuwa katika hatari kubwa ya kukosa maarifa sahihi kuhusu lishe.

Kwa upande mwingine, wagonjwa waliokuwa na shinikizo la damu pekee walionekana kuwa na uelewa mzuri zaidi wa lishe kuliko wale waliokuwa na kisukari na shinikizo la damu kwa pamoja.

Watafiti wanasema lishe bora, ni sehemu muhimu ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza. Mbali na matumizi ya dawa, uchaguzi wa chakula unaofaa, unaweza kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, kupunguza shinikizo la damu na kupunguza hatari ya kupata matatizo kama vile kiharusi, magonjwa ya moyo na kushindwa kwa figo.

Kutokana na matokeo hayo, watafiti wanashauri kuwepo kwa programu maalumu za elimu ya lishe zinazolenga wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, hususan makundi yaliyo katika mazingira magumu kiuchumi na kijamii.

Wanasema elimu hiyo inapaswa kuzingatia mazingira halisi ya Tanzania, ili iwe rahisi kwa wagonjwa kuelewa na kutekeleza ushauri wa lishe katika maisha yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa hitimisho la utafiti, kuboresha uelewa wa lishe miongoni mwa wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, kutasaidia kuongeza uwezo wao wa kujitunza, kuboresha matokeo ya matibabu na kupunguza mzigo wa magonjwa hayo kwa familia na mfumo wa afya nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *