
Kocha wa Simba, Steve Barker jana ametinga katika mazoezi ya kikosi cha wanawake cha klabu hiyo na kutoa ahadi mbili ambazo yeye na wasaidizi wake watazifanyia kazi.
Ahadi ya kwanza ni kujitokeza katika mechi zao kila anapopata nafasi na ya pili ni makipa wa Simba Queens kufanya mazoezi ya pamoja na wale wa kikosi cha wakubwa cha Simba ili kuwaongezea ubora.
“Sijakaa hapa kwa muda mrefu ni takribani dakika 10 kwa ajili ya kuwapa sapoti kama nyie mnavyotoa sapoti kwa kikosi cha wakubwa. Ubora ninaouona ni wa hali ya juu. Namna mnavyocheza kwa nguvu, kwa ari na kwa ushindani imenivutia sana.
“Nimefurahishwa kwa kiwango hiki cha juu. Hongereni kwa kazi nzuri na nawatakieni kila la kheri. Tutajaribu kutafuta muda ambao hatutakuwa na mechi kuja kuwatazama na kuwapa sapoti, labda Kocha wa makipa atawachukua makipa kwa awamu moja au mbili na kufanya nao mazoezi,” amesema Barker.
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Musa Hassan ‘Mgosi’ amesema kuwa amefurahishwa na namna Barker anavyowaunga mkono.
“Nimefurahishwa na jambo hili kwa sababu mara ya kwanza tunakutana naye katika utambulisho alionyesha toka mwanzo alionyesha ni mtu ambaye anahitaji timu zote za Simba zinafanya vizuri.
“Kwetu sisi tumefarijika. Wachezaji wamefurahi sana kwa kile ambacho kimefanyika. Ni kitu ambacho kimeonyesha morali kubwa sana katika timu,” amesema Mgosi.
Beki wa Simba Queens, Fatuma Issa ‘Densa’ amesema Barker na benchi lake la ufundi wamewapa hamasa.
“Hiki kitu tulikuwa tunakiona katika nchi za Ulya zilizoendelea. Kocha kupata nafasi kuja kutufundisha ni jambo zuri kwetu maana litatuongezea maarifa,” amesema Densa.
Simba Queens inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa na pointi 31 ilizokusanya katika mechi 11, ikifuatiwa na Yanga Princess yenye pointi 30.