Marekani. Staa wa muziki na filamu kutoka Marekani, Selena Gomez amesema ndoa yake na mtayarishaji maarufu wa muziki Benny Blanco imejengwa katika misingi ya upendo, kuheshimiana na kuelewana.

Gomez alifunguka hayo alipoalikwa katika kipindi cha mazungumzo ya maisha kiitwacho ‘Friends Keep Secrets podcast’, kinachoendeshwa na mumewe Blanco akishirikiana na mastaa Lil Dicky na Kristin Batalucco.

Katika mahojiano hayo, alisema harusi yao ilikuwa moja ya siku bora zaidi katika maisha yake na ilithibitisha namna wanavyothaminiana kama wenzi wa maisha.

“Ni moja ya siku bora zaidi kuwahi kutokea katika maisha yangu, nafurahia ndoa yangu kwa sababu ina afya na tunapendana na kuheshimiana sana hilo ndilo jambo la msingi,” alisema Gomez.

Hata hivyo, kilichovutia zaidi hisia za mashabiki ni tukio la

Gomez kuonekana akimbusu na kuugusa kwa upole mguu wa Blanco kama ishara ya mapenzi, kitendo kilichowaacha mashabiki wengi wakiwa na mshangao, pia kikiibua mjadala mkubwa mitandaoni.

Tukio hilo lilitokea dakika ya 48 ya kipindi hicho na mara moja likaanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii huku mashabiki wakitoa maoni tofauti kuhusu wawili hao wanavyoonyesha mapenzi yao hadharani.

Siku chache kabla ya tukio hilo, Blanco alikuwa gumzo mtandaoni baada ya kuonekana akiweka miguu yake juu ya kochi kwenye sehemu ya kwanza ya kipindi hicho, huku nyayo zake zikiwa chafu.

Baadaye alijitetea alipokuwa akizungumza katika kipindi cha televisheni cha Jimmy Kimmel Live! ilikuwa ni bahati mbaya tu ya muda na kusisitiza ana miguu misafi.

Kitendo cha Gomez kumbusu mguu wa mumewe kimeonekana na wengi kama ishara ya mapenzi makubwa kati yao, huku wengine wakiona ni namna ya kipekee ya kumtetea Blanco dhidi ya mzaha uliokuwa unaendelea mitandaoni.

Wawili hao walianza uhusiano wa kimapenzi mwaka 2023 baada ya kuwa marafiki na washirika wa muda mrefu katika muziki. Kabla ya kuchumbiana, waliwahi kufanya kazi pamoja katika baadhi ya miradi ya muziki, jambo lililowafanya kuwa karibu zaidi.

Baadaye walithibitisha hadharani wako kwenye uhusiano, hatua iliyowafurahisha baadhi ya mashabiki wao wengi. Haikuchukua muda mrefu na mwaka 2024 walitangaza wamechumbiana rasmi.

Mwaka mmoja baadae  walifunga ndoa katika sherehe ya faragha Marekani, wakianza maisha mapya ya ndoa pamoja hadi hii leo ikiwa inakaribia mwaka sasa tangu wafunge pingu za maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *