Chanzo cha picha, Getty Images/BBC
Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Iran kujisalimisha bila masharti huku mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel yakiendelea. Trump amesema baada ya Iran kuchagua uongozi mpya unaokubalika na Washington, Marekani na washirika wake wataisaidia nchi hiyo kuimarisha uchumi wake.
Kauli hiyo imekuja wakati vita vinaingia wiki ya pili tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei katika mashambulizi ya hivi karibuni. Hata hivyo bado haijulikani nani ataIongoza Iran baada ya tukio hilo.
Ikulu ya Marekani imesema operesheni za kijeshi zinaweza kudumu kati ya wiki nne hadi sita, huku lengo likiwa kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran.
Wakati huo huo, rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa simu na rais wa Iran Masoud Pezeshkian, akitoa pole kwa vifo vilivyotokea katika mashambulizi hayo.
Urusi imesisitiza kuwa mapigano yanapaswa kusitishwa mara moja na kutafutwa suluhisho la kidiplomasia. Iran nayo imeishukuru Urusi kwa kuendelea kuiunga mkono.
Wakati huo huo, mapigano yameongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kundi la Hezbollah kushambulia Israel, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yakiripotiwa katika nchi kadhaa zenye kambi za kijeshi za Marekani.