London, England. Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior amesema hawezi kubadilishana mshambuliaji mwenye moto, Joao Pedro na mchezaji yeyote duniani kwa sasa.

Hat-trick ya Mbrazili huyo katika Uwanja wa Villa Park imefanya atoke kwenye mazungumzo ya kuwa usajili bora wa majira ya joto hadi kuanza kutajwa kama mmoja wa washambuliaji bora duniani.

Msimu huu ni Erling Haaland, Harry Kane na Kylian Mbappé pekee ndio waliomzidi Joao Pedro kwa kufunga mabao yasiyo ya penalti.

Si hivyo tu. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amefunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu England mwaka 2026 kuliko mchezaji mwingine yeyote. Na katika ligi tano bora barani Ulaya, ni Harry Kane pekee aliyemzidi mabao katika mwaka huu wa kalenda hadi sasa.

Mbrazili mwenzake Igor Thiago ndiye anayemkaribia zaidi kwa mabao saba, wakati Antoine Semenyo, Erling Haaland na mchezaji mwenzake wa Chelsea, Cole Palmer wakiwa na mabao sita kila mmoja.

Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, akimpongeza mshambuliaji wake hatari, Joao Pedro baada ya mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa kumalizika Machi 4, 2026. Picha na Mtandao

Kocha Rosenior aliulizwa katika mkutano wake wa waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Wrexham A.F.C. kama angekubali kumbadilisha Pedro moja kwa moja na Haaland na kama Mbrazili huyo yuko katika kiwango sawa na Haaland, Mbappe na Kane.

Rosenior alisema: “João sasa yuko katika kundi hilo. Katika miezi miwili ambayo nimekuwa hapa, ameonyesha mara kwa mara kwamba yeye ni mshambuliaji wa kiwango cha dunia. Ninapenda kuzungumzia wachezaji wangu. Si vizuri kumlinganisha na Erling kwa sababu ni kukosa heshima. Simfahamu sana binafsi, lakini najua kwa ninachoona kutoka nje kwamba yeye pia ni mshambuliaji wa kiwango cha juu sana. Kwa kweli, kwa sasa singembadilisha João na mchezaji yeyote.”

Pedro amejiwekea lengo la kufunga mabao sita zaidi ya ligi katika mechi tisa zilizobaki za Chelsea msimu huu. Aliliambia SunSport kuhusu azma yake ya kuwa mshambuliaji wa kwanza kufunga mabao 20 ya ligi katika msimu mmoja kwa Chelsea tangu Diego Costa afanye karibu miaka kumi iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *