Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, nchini Uswisi, Türk amebainisha kuwa raia wamekuwa wakilengwa kwa makusudi, “Raia wanauawa kikatili, wanajeruhiwa na kufurushwa kila siku nchini Sudan Kusini huku uhasama ukizidi kati ya jeshi na vikosi vya upinzani. Baadhi ya vitendo hivi ni sawa na uhalifu wa kivita.”
Ndani ya siku 17 zilizopita, zaidi ya raia 160 wameuawa kikatili katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mauaji ya watu 139 huko Abiemnom yaliyofanywa na wapiganaji wa kabila la Bul Nuer Machi 1, 2026.Amesema hali ni mbaya zaidi kwani ripoti zinaonesha kuwa majeshi ya serikali ya Sudan Kusini yamekuwa yakiharibu au kutia sumu vyanzo vya maji vya umma.
Wanawake wakipokea huduma katika hopitali ya Kaunti ya Akobo jimboni Jonglei Sudan Kusini
Mauaji ya kikatili
Katika tukio la kusikitisha la Februari 21, 2026 huko Pankor, mjini Ayod, Türk amesema wanajeshi wamewauwa raia 21 baada ya kuwahadaa kuwa wanakusanywa ili kupewa misaada ya chakula.
Miongoni mwa waliouawa, wanawake 15 na wasichana watatu wamepoteza maisha baada ya kufyatuliwa risasi ghafla, huku wengine wakiripotiwa kukatwa vichwa katika jimbo la Western Bahr al Ghazal.
Türk amesisitiza kuwa, “Lazima kuwe na uchunguzi wa haraka, usio na upendeleo, wa kina na wenye tija kuhusu ukiukwaji huu wa sheria za vita. Na wale watakaopatikana na hatia lazima wawajibishwe kikamilifu.”
Volker Türk amesisitiza kuwa vitendo vya kuharibu visima vya maji takriban 99 kwa sumu au mashambulizi ya anga ni kosa la jinai ambalo lazima lichunguzwe.
Tangu mwezi Desemba mwaka jana, zaidi ya watu 280,000 wamepoteza makazi yao katika majimbo ya Jonglei, Lakes, na Upper Nile kutokana na mapigano haya yanayozidi kupamba moto. Hali ya usalama imezidi kuzorota kufuatia amri ya jeshi la Sudan Kusini ya Machi 6, 2026 inayowataka raia wote kuondoka mji wa Akobo, huku wakitaka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS, na mashirika ya msaada kuondoka pia.
Walinda amani wamekataa kuondoka ili kuendelea kuwalinda raia, ingawa maelfu ya watu tayari wamekimbia mji huo kwa hofu ya kuanza kwa mapigano makubwa.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaandamana na wataalamu wa haki hadi Mundri katika eneo la mbali la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini.
Wito wa Umoja wa Mataifa
Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja ili kuokoa maisha ya watu na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wenye uhitaji bila vikwazo na kuwataka viongozi wa pande zote mbili kurudi kwenye meza ya mazungumzo ili kuunusuru mkataba wa amani ambao kwa sasa upo hatarini kusambaratika kabisa.
“Lazima kuwe na usitishaji mapigano haraka iwezekanavyo, ili kuokoa maisha na kuelekeza mzozo huu kwenye suluhu ya mazungumzo,” amesema bwana Türk.
