Mashirika hayo yanaonya kuwa kuongezeka kwa mgogoro Mashariki ya Kati tayari kunachochea harakati mpya za watu kuvuka mipaka, huku familia nyingi zikiwasili zikiwa zimechoka baada ya safari ndefu, ngumu na bila kujua mustakabali wao.
Familia zinawasili zikiwa ziko taaban
Akizungumza mjini Geneva, Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan, Tajudeen Oyewale, amesema wafanyakazi wa misaada wanashuhudia hali ya huzuni na uchovu mkubwa miongoni mwa familia zinazowasili katika vituo vya mapokezi.
“Tayari tunaona akina mama wengi wakifika katika vituo vya mapokezi wakiwa na watoto wao, wamechoka sana, wameelemewa na wanahitaji msaada wa haraka,” amesema.
Oyewale ameonya kuwa ikiwa idadi ya wanaowasili itaongezeka kama inavyotarajiwa, “hatari zinazowakabili watoto zitaongezeka pia.”
Watoto ndio wanaoathirika zaidi
Mashirika ya kibinadamu yanasema watoto hasa wale wanaosafiri bila wazazi au walezi ndio walio katika hatari kubwa zaidi wakati wa uhamaji.
“Watoto wanahitaji uangalizi maalum, hasa wale ambao hawaandamani na mtu yeyote,” Oyewale amesisitiza, akionya kwamba bila hatua za ulinzi wanaweza kukumbwa na “hatari kubwa za ulinzi, ikiwa ni pamoja na kutekwa na vitendo vya ukatili.”
Katika kilele cha kurejea kwa wakimbizi mwaka uliopita, UNICEF imewasaidia zaidi ya watoto 8,000 waliokuwa wametengana na familia zao au kusafiri peke yao waliorejea Afghanistan kutoka Iran na Pakistan.
Raia wengi wa Aghhanistan waliorejea karibuni kutoka Iran wanategemea msaada wa chakula wa UN ili kuishi
Mfumo wa msaada wa kibinadamu umelemewa
Kurejea huku kunatokea wakati Afghanistan tayari inakabiliwa na changamoto kubwa za kibinadamu.
Takribani Waafghan milioni tatu walirejea kutoka nchi jirani mwaka 2025, ambapo karibu asilimia 60 walikuwa familia zenye watoto.
Wakati huo huo, nchi hiyo inakabiliwa na migogoro mingi kwa wakati mmoja, huku watoto milioni 11 wakihitaji msaada wa kibinadamu.
Mashirika hayo ya misaada yanasema kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji kunafanya hali kuwa ngumu zaidi.
“Utoaji wa huduma za msingi unacheleweshwa kwa mfano, watoto wenye utapiamlo hawawezi kupata chakula maalum cha tiba kinachookoa maisha kwa wakati,” amesema Oyewale.
Wito wa dharura kwa msaada wa kimataifa
UNICEF na UNHCR zinasema zinafanya kazi na washirika kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika maeneo ya mpakani na katika jamii ambazo familia zinarejea, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, chanjo, uchunguzi wa lishe na ulinzi wa watoto.
Hata hivyo, mashirika hayo yanaonya kuwa mpango wa kukabiliana na hali ya kibinadamu Afghanistan unakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha.
“Hatua za mapema ni muhimu ili kuhakikisha kwamba iwapo idadi ya wanaorejea itaongezeka, watoto na familia wanaweza kupata msaada kwa wakati na huduma muhimu,” amesema Oyewale.
Ametoa wito wa dharura kwa wafadhili na washirika kusaidia kusafirisha kwa ndege vifaa muhimu vya lishe, afya na usafi, akisisitiza, “Ujumbe wetu ni rahisi watoto lazima walindwe na kusaidiwa katika kila hatua wanapohitaji msaada wetu zaidi.”
