NAIROBI – Kenya na Afrika Kusini zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika sekta ya teknolojia na mawasiliano ya kidijitali ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili mnamba (AI) na kuenea kwa taarifa za kupotosha mtandaoni.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Haya ni kwa mjibu wa kaimu naibu mkurugenzi wa Idara ya mawasiliano ya serikali ya Afrika Kusini Sandy Lenene, wakati wa mahojiano na RFI Kiswahili jijini Nairobi, pembezoni mwa mkutano wa matumizi salama ya mtandao wa Tiktok uliowaleta pamoja wadau wa teknolojia, serikali na mashirika ya kimataifa kujadili usalama wa mtandao.
Lenene amesema ziara ya ujumbe wa serikali ya Afrika Kusini nchini Kenya inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, hasa katika masuala ya uchumi wa kidijitali na mawasiliano ya serikali.
Kupambana na taarifa potofu
Baadhi ya mwaswala yaliyojadiliwa wakati wa mkutano huo ni namna ya kukabiliana na kuenea kwa taarifa ghushi na maudhui hatari kwenye mitandao ya kijamii.
Lenene amesema serikali nyingi duniani zinakabiliwa na changamoto ya kuenea kwa taarifa zisizo sahihi, hasa katika zama za maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba.
“Katika zama za AI, swali ni jinsi gani tunaweza kuwasiliana vizuri zaidi na raia na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, huku tukidhibiti maudhui hatari kama vile picha ghushi na taarifa za akili mnemba,’’
Ameongeza kuwa serikali za Afrika zinahitaji kushirikiana na makampuni ya teknolojia kama TikTok na Meta ili kuweka mifumo madhubuti ya kulinda usalama wa watumiaji wa mtandao.
Elimu ya matumizi ya kidijitali
Kadhalika kaimu huyo naibu mkurugenzi wa Idara ya mawasiliano ya serikali ya Afrika Kusini, alisisitiza umuhimu wa kuongeza elimu ya matumizi ya teknolojia kwa wananchi, hasa vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, akisema vijana wengi barani Afrika hutumia takribani saa nne kwa siku kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuwa fursa au changamoto kulingana na jinsi wanavyotumia muda huo. Aidha aliongeza kuwa serikali zinapaswa kuhamasisha vijana kutumia teknolojia kama chombo cha ubunifu, biashara na maendeleo ya uchumi.
Aliendlea na kusema bara la Afrika linapaswa kujikita zaidi katika kuunda na kuendeleza teknolojia badala ya kuwa watumiaji tu wa huduma za kidijitali zinazotengenezwa nje ya bara hilo
“Hatupaswi kuwa bara linalotumia tu maudhui ya kidijitali. Tunataka kuwa wabunifu, watengenezaji na wazalishaji wa teknolojia,” amesema.
Ushirikiano wa kihistoria
Kwa mujibu wa Lenene, Kenya na Afrika Kusini zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu, kabla na baada ya kuenea kwa matumizi ya mitandao.
Amesema Kenya imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mazingira ya ubunifu wa kidijitali.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kusaidia mataifa hayo mawili kuongoza juhudi za kuoanisha sera za uchumi wa kidijitali barani Afrika.
Kongamano la matumizi salama ya mtandao wa TikTok lililiwaleta pamoja wadau mbali mbali kutoka kote duniani kujadili matumizi salama ya mtandao huo.