ZILE vurugu zote za wapi mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Tanzania Prisons na Yanga itachezwa, zimezimwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyopangwa ipigwe Jamhuri, Dodoma huku wenyeji wa mechi hiyo, Tanzania Prisons kiroho safi wamekubali. Lakini ndani ya dakika tisini za mechi hiyo, kuna kitu.

Ushindi wa mechi tatu pekee kati ya 15 ilizocheza Prisons katika Ligi Kuu Bara msimu huu, inamuumiza kichwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Shadrack Nsajigwa ambaye leo Alhamisi saa 2:00 usiku ana kibarua cha kukiongoza kikosi hicho kucheza dhidi ya Yanga.

Nsajigwa aliyewahi kuichezea Yanga kuanzia 2006 hadi 2012 akiwa miongoni mwa mabeki tegemeo, anakutana na chama lake hilo la zamani huku akiwa na mtihani wa kuiokoa Prisons na janga la kushuka daraja ikishika nafasi ya 15.

Kwa upande wa Yanga, inaingia uwanjani ikiwa haijapoteza mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu kati ya 12 ilizocheza ikishinda kumi na sare mbili. Pia ndiyo timu yenye safu kali ya ulinzi ikiruhusu mabao mawili, pia imetikisa nyavu za wapinzani mara 30, ikiwa pia ndiyo timu iliyofunga mabao mengi katika ligi hiyo.

Prisons ina mlima mrefu wa kuupanda mbele ya Yanga kwani haijawahi kupata ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi tangu iliposhinda 2-0, Mei 10, 2018.

Mbaya zaidi, Prisons msimu uliopita ilifungwa jumla ya mabao 9-0 dhidi ya Yanga, baada ya mechi ya kwanza kupoteza kwa 4-0, kisha 5-0.

Akizungumzia mechi hiyo, Nsajigwa alisema: “Yanga ni mabingwa watetezi na pia wanaongoza msimamo wa ligi. Kukutana na timu kama hiyo kunahitaji dhamira na nidhamu katika muda wote wa mchezo.”

Alieleza kuwa, maandalizi yameathiriwa kidogo na mabadiliko ya ghafla ya uwanja ambapo awali walitakiwa kucheza Sokoine jijini Mbeya, lakini uwanja huo umefungiwa kwa kukosa vigezo vya kanuni, kisha wakaelekea Tabora kabla ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupanga mechi ichezwe Jamhuri, Dodoma.

Licha ya changamoto hizo, kocha huyo alisisitiza kuwa kikosi chake kinaendelea kuwa makini na kujiandaa kwa ajili ya mechi hiyo.

Tangu achukue rasmi jukumu la kuinoa klabu hiyo hivi karibuni, Nsajigwa ameisimamia katika mechi mbili akianza na Ligi Kuu Bara iliyoisha bila kufungana dhidi ya Azam, kisha kichapo cha 1-0 mbele ya TMA Stars katika Kombe la Shirikisho la CRDB. Zote ikiwa nyumbani.

Mechi ya leo Yanga itamkosa Dickson Job ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti akitarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili hadi mitatu. Hata hivyo, Pacome Zouzoua amerejea baada ya kukosekana kwenye mechi tano.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kitendo cha hadi juzi hakuwa na uhakika wa mechi hiyo itachezwa wapi, imeathiri kidogo maandalizi yake.

“Kwa bahati mbaya maandalizi yetu yameathiriwa kwa sababu hadi jana (juzi Jumanne) usiku hatukuwa tunajua tunakwenda kucheza wapi, lakini tunachoangalia zaidi ni kiwango cha timu yetu, tunawafahamu wapinzani wetu, lakini pia sehemu tunayokwenda kucheza itaathiri pia uchezaji wetu. Kubwa tumejiandaa na mechi hiyo.

“Kucheza na timu iliyopo katika nafasi za chini ni changamoto kwa sababu itafanya juhudi kujikwamua, lakini tumejiandaa kukabiliana na hali yoyote ile,” alisema Pedro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *