
Akiba ya mafuta ya Marekani imepungua hadi kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miaka 44 iliyopita, na hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.
Mtandao wa CBS wa Marekani umetangaza kuwa: Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umeamuru kuachiliwa kwa mapipa milioni 172 ya mafuta kutoka Hifadhi ya Kistratejia ya Petroli ya Marekani baada ya Iran kufunga Lango Bahari la Hormuz na hivyo kuibua tatizo la uhaba wa nishati katika soko la kimatifa. Uchambuzi wa data za Idara ya Nishati ya Marekani na CBS unaonyesha kuwa suala hilo limepunguza sana hifadhi ya mafuta ya Marekani na kuipelekea ifikie kiwango cha chini kabisa katika miaka 44 iliyopita.
Wakati huo huo, baada ya bei ya petroli kuongezeka kufuatia uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati zimekubali kutoa takriban mapipa milioni 400 ya mafuta kutoka kwenye hifadhi zao za kimkakati ili kupunguza shinikizo kwenye soko la mafuta duniani.
Kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefunga Lango-Bahari la Hormuz, ambayo ni njia muhimu ya uchukuzi na usafiri wa majini duniani, na hivyo kupelekea kuongezeka kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa.