
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema katika ujumbe kuwa: Watu wakubwa wa Iran kwa mara nyingine wameonyesha kwa hatua zao thabiti mitaani kwamba dhamiri iliyo macho ya taifa hili lenye busara dhidi ya dhulma haitanyamazishwa na tishio lolote.
Kwa mujibu wa Pars Today, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran katika ujumbe wake wa kupongeza uwepo wa shauku na hamasa wa wananchi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuitikia kwao wito wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kkiislamu, ametaja uwepo na mahudhurio hayo kuwa dhihirisho kubwa la ujasiri, utambuzi na uwajibikaji wa taifa kubwa la Iran.
Ujumbe huo unasema: ‘Uwepo huu wa kipekee umeonyesha kuwa taifa la Iran linaendelea kuwepo kwa nguvu katika medani za maamuzi ya hatima na kuchukulia kuwatetea wanaodhulumiwa na kusimama kidete dhidi ya dhulma na adui mchokozi katika hali yoyote ile kuwa jukumu lao la kihistoria na kibinadamu.
Ghalibaf amesema: Leo imethibiti kwa mara nyingine tena kwamba watu wa Iran daima wana nafasi ya uwajibikaji na yenye umuhimu mkubwa katika nyakati nyeti katika historia yao, na ujasiri huu, moyo wa mshikamano na mwamko unaweza kuunda mustakbali mwema kwa manufaa ya jamii na eneo.