
Brigedi za Shahidi Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) zimepongeza mashambulizi yaliyofanywa na Iran katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) katika kujibu mashambulizi ya kichokozi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tarifa ya Brigedi za Shahidi Izzuddin Qassam imesisitiza kuwa oparesheni ya makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) dhidi ya shabaha za Wazayuni inaonyesha uungaji mkono endelevu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Palestina na maeneo matukufu ya Kiislamu.
Msemaji wa Brigedi za Shahidi Izzuddin Qassam ametangaza kuwa: Tunapongeza mashambulizi ya makombora ya IRGC dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyofanywa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds kama sehemu ya mashambulizi endelevu dhidi ya utawala huo kwa kutumia makombora ya kisasa.
“Mashambulizi hayo yamepoza nyoyo zetu zilizojeruhiwa na yamezitia moyo nyoyo za wapigania ukombozi na uhuru kote duniani kabla ya kuwasha moto katika anga ya Tel Aviv,” imeeleza taraifa ya Brigezi za Izzuddin Qassam.
Abu Obeida amesema kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds imeshuhudia mamilioni ya wananchi wa Iran wakiwa mitaani kwa ajili ya kuutetea na kuuhami Msikiti wa al Aqsa licha ya vita vya kulazimishwa vya madola ajinabi dhidi yao.
Amesema: Kushiriki mamilioni ya wananchi azizi wa Iran katika maandamano ya nchi nzima kwa ajili ya kuunga mkono na kuuhami Msikiti wa al Aqsa licha ya vita vikali vinavyoendelea dhidi yao na kujiunga katika maandamano ya jana viongozi wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu kunadhihirisha msimamo thabiti wa wananchi na viongozi wa Iran wa kuitetea Palestina.
Amesema, ushiriki mkubwa wa hamasa wa wananchi wa Iran katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds pia unaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chini ya uongozu wa Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, inaendeleza njia ileile iliyoaainishwa kwa damu na mtangulizi wake, Ayatullah Ali Khamenei.
Abu Obeida ameongeza kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa ya kuuunganisha Umma wa Kiislamu na kuelekeza upya jitihada zake katika masuala muhimu ya Umma.