Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na namna fedha za Bajeti ya Mwaka 2025/2026 zilizoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinavyotumika katika utekelezaji wa Miradi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati pamoja na zoezi la kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kitongoji cha Mine, kata ya Mwakata, Jimbo la Msalala na kitongoji cha Mjimwema katika Jimbo la Kahama wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, amesema ziara ya kamati imelenga kukagua na kujionea utekelezaji wa Miradi ili kuhakikisha fedha zilizotengwa na Bunge zinatumika kwa ufanisi.

“Tumepewa dhamana na Bunge kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatekeleza kusudi lililokusudiwa. Bunge lilitenga bajeti ya shilingi bilioni 400 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya miradi ya kufikisha umeme vitongojini, na tumekuja kuona thamani ya fedha hizo kama imetumika ipasavyo. Kwa kweli tumeridhishwa na kazi inayofanywa na REA,” amesema Mhe. Mgalu.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya umeme.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema ukaguzi wa miradi unaofanywa na Kamati ya Bunge ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Katiba, inayolenga kuhakikisha Bunge linasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo.

Makamba amesema katika bajeti ya Wizara ya Nishati, ilipanga kuwa kila jimbo nchini litapatiwa vitongoji 15 vitakavyofikishiwa huduma ya umeme ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa Wananchi.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *