Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu ununuzi wa mabati yasiyokidhi viwango yaliyokusudiwa kutumika katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Katavi (Katavi Boys), hatua iliyosababisha Serikali kutoa fedha mara mblii.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Machi 16, 2026, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Maridadi, Mpanda Mjini mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alihoji mchakato wa ununuzi wa mabati takribani 4,000 yenye thamani ya karibu shilingi milioni 198, ambayo yalibainika kuwa hayakukidhi viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

“Takribani milioni 200 zimenunua mabati yasiyofaa. Nani aliagiza haya mabati? Kwa nini Serikali itoe fedha mara mbili kwa jambo hilo?” alihoji Waziri Mkuu.

“Mkandarasi aliyeleta mabati hayo na watumishi wote waliohusika wakamatwe mpaka fedha ya Serikali irudi, na wachukuliwe hatua za kisheria.”

Aidha, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Sipha Nkusi Mwanjala, kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ushiriki wa kila mtu katika mchakato wa manunuzi hayo.

Mkandarasi (Mzabuni) aliyesambaza mabati hayo ni kampuni ya Resa Roofers Limited ya jijini Mwanza inayomilikiwa na Samwel Richard.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *