DAR ES SALAAM: MRADI wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mzizima Towers unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefikia asilimia 91 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Desemba 31, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano,Deus Sangu alieleza hayo Machi 16,2025 Dar es salaam alipowasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Awali, Katika taarifa yake Sangu alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa rasmi mwaka Aprili 2013 na ulitarajiwa kukamilika Machi 2017 lakini kutokana na changamoto mbalmbali haukuweza kujamilika kwa muda lakini umefikia asilimia 91 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31,2026.

“Sababu ya kuchelewa mradi huu ulisimamishwa kupisha ukaguzi wa SSRA na BOT mwaka 2016 na kufuatia ukaguzi wa PPRA kuanzia mwaka 2019 hadi 2022, pia ulichelewa kwa sababu ujenzi wa hoteli ulianza bila uteuzi wa mwendesha hoteli,” alisema Sangu.

Aliongeza sababu nyingine ni kuwa kibali kilivyotoka kulikuwa na janga lililolikumba dunia la UVIKO -19 ambalo liliathiri sekta ya hoteli kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, pia walichelewa kumpata msanifu wa ndani wa hoteli na mabadiliko ya usajili kwa hoteli hiyo kuwa na hadhi ya nyota tano.

Sangu alisema mradi huo ni wa uwekezaji unahusisha ujenzi wa minara miwili, ikiwemo mnara wa biashara wenye ghorofa 35 na mnara wa makazi wenye ghorofa 32, ukiwa na jumla ya eneo la ujenzi la mita za mraba 95,018.15.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, alisema wajumbe wa kamati wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua mradi huo uendelee kutekelezwa ili uweze kuleta tija kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla.

“Sisi kamati tumefika hapa na kujionea kazi inayofanyika katika mradi huu. Kazi ni nzuri sana na inaonesha kuwa uongozi wa NSSF chini ya Mkurugenzi Mkuu, Masha Mshomba, umekuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi,” alisema Hawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *