LINDI: SERIKALI imezindua Jukwaa la Majadiliano ya Biashara kwa Biashara (B2B) likiwa na lengo la kuchochea uwekezaji, kuongeza thamani ya rasilimali za misitu na kuimarisha uhifadhi nchini, huku ikisisitiza kuwa misitu ni msingi wa maisha na uchumi endelevu.

Uzinduzi huo umefanyika Machi 18, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi, ukiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti inayofanyika kila mwaka Machi 21.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, katika uzinduzi huo amesema uhifadhi wa misitu si chaguo bali ni hitaji la msingi kwa ustawi wa binadamu na uchumi wa taifa.

“Bila kuhifadhi hatuna maji, bila kuhifadhi hatuna maisha. Tunapozungumzia uhifadhi, tunazungumzia uhai wa binadamu na mustakabali wa vizazi vijavyo,” amesema Telack.

Amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau wa sekta ya misitu, wafanyabiashara na serikali ili kujadili namna bora ya kutumia rasilimali hizo kwa tija bila kuathiri mazingira.

Katika hatua nyingine, Telack amesisitiza  umuhimu wa mkoa huo katika sekta ya misitu akibainisha uwepo wa  mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya misitu, ikiwemo mbao ngumu na mikorosho.

“Mkorosho ni msitu. Tukikata mikorosho na kuona maghorofa pekee, ujue tumefilisika,” ameonya Telack.

Amepongeza  juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na upandaji miti nchini akimtaja kuwa kinara wa ajenda hiyo.

Kwa upande wake, msimamizi wa mjadala huo, Dk Siima Bakengesa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema jukwaa hilo linalenga kuunganisha fursa za biashara kupitia mifumo ya B2B na B2G ili kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika uchumi.

“Hapa tunalenga kuweka mazingira wezeshi ili sekta ya misitu na nyuki iweze kutoa thamani kubwa zaidi kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Dk Bagengesa.

Ameongeza kuwa mada nane zimeandaliwa kujadili masuala muhimu ikiwemo biashara ya kaboni, matumizi ya teknolojia, sera na kanuni pamoja na namna ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.

Uzinduzi huo unatangulia tukio kubwa la kitaifa la ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa, unaotarajiwa kufanyika Machi 19, 2026 katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi .

Mgeni rami  katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais ,Dk Emmanuel Nchimbi, atakayeongoza uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya upandaji miti.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa,” yakilenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi na wadau katika uhifadhi wa misitu na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *