Shambulio hilo, lililotekelezwa jioni ya Jumatano, Machi 18, huko Tiné, mji ulioko mashariki mwa Chad kwenye mpaka na Sudan, linahusishwa na ndege isiyo na rubani ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ambao wanapigana na jeshi la Sudan tangu mwezi Aprili 2023. Kufuatia mkutano wa baraza la ulinzi na usalama uliofanyika usiku, Rais wa Chad Mahamat Idriss Déby aliagiza jeshi la Chad “kulipiza kisasi dhidi ya shambulio lolote linalotoka Sudan.”

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Ndege isiyo na rubani kutoka Sudan iliwaua watu 17 na kuwajeruhi vibaya watu kadhaa jioni ya Jumatano, Machi 18, katika mji wa Tiné, nchini Chad. Kulingana na chanzo cha kijeshi kilichothibitisha tukio  hilo kwa shirika la habari la AFP, shambulio hilo lilitekelezwa na ndege isiyo na rubani ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), kundi la wanagambo linalopigana na jeshi katika nchi jirani ya Sudan.

“Hatujaweza kumtambua mhalifu,” ameeleza Gassim Chérif, Waziri wa Mawasiliano, kwa mwandishi wetu huko N’Djamena, Nadia Ben Mahfoudh. ” Ni shambulio la ndege zisizo na rubani, na walengwa walikuwa raia wa Chad katika eneo la ukumbusho, eneo la mazishi. Kwa hivyo, kwa sasa, hatujaweza kumtambua mhalifu. Uchunguzi unaendelea ili kubaini ni nani aliye nyuma ya shambulio hili la ndege zisizo na rubani.”

Msemaji wa serikali ya Chad amelaani shambulio hilo, akisema: “Hii si mara ya kwanza kwa aina hii ya shambulio la kikatili na la kutisha kufanywa dhidi ya raia wa Chad wasio kuwa na hatia.” Msimamo wa Chad umekuwa kila mara kuwataka wapiganaji mbalimbali kuweka kipaumbele mazungumzo, amani, na mashauriano.

Haki ya kujibu

Gassim Chérif ameongeza: “Tumetoa maonyo. Licha ya hatua zote zilizochukuliwa, pande mbalimbali zimeendelea kukiuka eneo la Chad, na kwa hivyo vikosi vya ulinzi na usalama vimetumwa. Sasa vinawekwa ili kutekeleza haki ya kulipiza kisasi kwa mujibu wa sheria ya kimataifa: yaani, kuingia katika eneo la Sudan kuwafuatilia wahusika na washirika wa vitendo hivi viovu na vya kikatili dhidi ya raia wa Chad.”

Tangu Aprili 15, 2023, mzozo nchini Sudan kati jeshi la Jenerali al-Burhan dhidi ya wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vya Jenerali Hemedti. Katika miezi ya hivi karibuni, vita hivi vimeenea mara kwa mara katika eneo la Chad. Mwishoni mwa mwezi Februari, kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara, serikali ya Chad iliamua kufunga mpaka wake wa karibu kilomita 1,400 na Sudan.

Kwa upande wao, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimekana kuhusika kwa shambulio hilo siku ya Alhamisi, Machi 19, kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, vikiwashutumu wapinzani wao wa jeshi la Sudan: “Vikosi vya Msaada wa Haraka vinalaani kwa nguvu zote shambulio la kigaidi lililofanywa siku ya Jumatano na tawi la kijeshi la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) kwa kutumia ndege zisizo na rubani, ambazo zililenga mji wa Tina katika Jamhuri ya Chad na kusababisha vifo vya raia kadhaa wasio na hatia.” »

Kati ya Chad na Sudan, mpaka wenye vinyweleo na mgumu kudhibiti

Rais wa Chad Mahamat Idriss Déby aliitisha mkutano wa baraza la ulinzi na usalama siku ya Jumatano usiku, akiagiza jeshi la Chad “kulipiza kisasi, kuanzia usiku wa leo, dhidi ya shambulio lolote linalotokana na Sudan,” kulingana na chapisho kutoka kwa ofisi ya rais kwenye mitandao ya kijamii.

Mwishoni mwa Februari, roketi iliyofyatuliwa kutoka Sudan ilisababisha uharibifu huko Tiné, ambapo wanajeshi 15 na raia 8 walipoteza maisha tangu mwisho wa mwezi Desemba kutokana na mzozo huo, kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP.

Darfur, eneo kubwa magharibi mwa Sudan linalopakana na mpaka, limekuwa karibu likidhibitiwa kabisa na wanajeshi wa RSF tangu kutekwa kwa mji wa El-Fasher mwezi Oktoba mwaka uliyopita. Mnamo Februari 21, walidai kuteka mji wa mpakani wa Tina, uliounganishwa na Tiné huko Chad, ambao umetenganishwa tu na sehemu nyembamba ya mto ambao kwa kiasi kikubwa ni mkavu.

Nchini Sudan, vita vya wenyewe kwa wenyewe vimewaua makumi ya maelfu ya watu na kusababisha zaidi ya milioni 12 kuhama makazi yao, wakiwemo karibu milioni moja huko Chad, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *