
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya raia 500 waliuawa nchini Sudan kati ya mwezi Januari na Machi, wakiwa kutoka eneo la Kordofan, kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, kupitia msemaji wake Marta Hurtado, imesema mashambulio kwa kutumia ndege zisizo na rubani yameendelea huku silaha pia zikitumika kwa urahisi katika maeneo yenye watu wengi, hali iliyochangia idadi hiyo ya vifo.
Aidha, ameongeza kwamba kwa majuma mawili ya mwanzo ya mwezi huu, zaidi ya raia 277 wameuawa kupitia mashambulio ya angani, ambapo watu 70, wakiwemo watoto 13, waliuawa wakiwa katika hospitali ya El Daein juma lililopita.
Jimbo la Kordofan kwa sasa ndilo uwanja wa mapambano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa RSF, kwani linaunganisha eneo la magharibi mwa Darfur, ngome ya wapiganaji wa RSF.
Zaidi ya watu milioni 11 nchini Sudan wamekimbia makwao na wengine maelfu kuuawa, wadadisi wakisema mapigano ya Sudan yamesababisha hali ya kibinadamu ambayo haijawahi kurekodiwa.