
Nchi ya Eritrea juma hili itamaliza miaka 18 ya kujitenga na Kombe la Mataifa ya Afrika wakati watakapowakaribisha Eswatini katika jiji la Morocco la Meknes kwa ajili ya mechi ya kwanza ya kufuzu kwa mashindano ya mwaka 2027.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kutoshiriki kwao mechi za kimataifa, kuliifanya FIFA kuiondoa nchi hiyo kwenye orodha ya nafasi za timu za taifa kidunia.
Mchezo huu ambao utachezwa kwenye uwanja wa d’Honneur nchini Morocco, ulihamishwa toka kwenye taifa hilo la pembe ya Afrika kutokana na viwanja vyake kukosa hadhi ya kimataifa.
Wakiwa wanafahamika kwa jina la utani ‘Ngamia wa Bahari nyekundu’, taifa hilo la Afrika Mashariki halijacheza kwenye michuano ya timu za taifa tangu mwaka 2008.
Tangu wakati huo, viongozi wa shirikisho la soka la Eritrea hawajawahi kutoa sababu za kukosekana kwao kwenye michuano mikubwa ya Afrika, lakini inaaminika kuwa ni kutokana na wachezaji wake kuwa wanaomba hifadhi pindi wanapocheza nje ya nchi yao.
Umoja wa Mataifa unaamini kuwa zaidi ya wachezaji na makocha 80 waliikimbia nchi yao, kwa kile walikitaja kukwepa ukandamizwaji wa kisiasa na kutumikia jeshi kwa muda mrefu.
Eritrea imekuwa ikiongozwa na rais Isaias Afwerk tangu ilipopata uhuru wake toka kwa Ethiopia mwaka 1993, mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiutaja utawala wake kama wakimabavu.
Licha ya kukosa mazoezi ya pamoja na mechi za kirafiki, Eritrea iliwaita wachezaji 24 wakiwemo 10 wanaocheza ligi ya nyumbani na wengine kutola Australia, Misri, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Ufilipino na Uswidi.