WANAWAKE wanaokumbwa na changamoto ya kuondolewa matiti kufuatia ugonjwa wa Saratani ya Matiti sasa wanatarajiwa kunufaika na msaada wa matiti bandi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya MNH, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dk Faraja Chiwanga, amesema msaada huo ni muhimu kwa wagonjwa kwani utawasaidia kurejesha hali yao ya kujiamini baada ya kufanyiwa matibabu.

“Tunatoa pongezi za dhati kwa Umoja Pharmaceuticals kwa moyo wao wa kujali. Wagonjwa wa saratani ya matiti hupitia changamoto kubwa si tu kimwili bali pia kisaikolojia, hivyo msaada huu utasaidia kuwapa faraja na kuimarisha hali yao ya maisha,” amesema.

Ameongeza kuwa hospitali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na msaada unaohitajika katika kila hatua ya matibabu yao. SOMA: MOI kufanya upasuaji wa saratani ya ubongo

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Pharmaceuticals, Lucy Lushiku, amesema kampuni hiyo imeguswa na changamoto wanazokutana nazo wagonjwa wa saratani ya matiti, hususan baada ya kufanyiwa upasuaji, na hivyo kuona umuhimu wa kuwasaidia wanawake hao. “Sisi tunaamini kuwa afya si matibabu ya mwili pekee, bali pia ustawi wa kisaikolojia. Ndiyo maana tumeamua kutoa msaada huu ili kuwasaidia wanawake hawa kurejesha tabasamu lao,” amesema.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kibingwa ikiwemo matibabu ya saratani ya matiti, huku ikijikita katika huduma jumuishi zinazohusisha matibabu, ushauri nasaha na ufuatiliaji wa wagonjwa baada ya matibabu.Msaada huo umetolewa na Umoja Pharmaceuticals wenye thamani ya shilingi milioni 400 ukiwa na lengo la kuboresha hali za kisaikolojia na maisha ya wanawake hao baada ya matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *