
Dar es Salaam. Jitihada za Tanzania kuvutia uwekezaji mkubwa zimepata msukumo mpya baada ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, kubainisha kuwa miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 7.8 (takribani Sh trilioni 20) kupitia Taasisi ya Bima ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI).
Balozi Omar alisema hayo wakati akifungua mkutano wa bodi ya taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kuwa serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kifedha unaolenga kupunguza athariza uwekezaji ambapo kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa fedha kwa miradi mikubwa ya maendeleo.
Alifafanua kuwa taasisi hiyo ni mshirika muhimu katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania, hasa katika kipindi ambacho nchi inashuhudia ongezeko la kubwa la wawekezaji.
“Tanzania kunahitaji ushirikiano imara unaoweza kuhamasisha mitaji kwa kiwango kikubwa. ATIDI ni mshirika muhimu kwa kusaidia kupunguza athari za kiuwekezaji, kuvutia uwekezaji binafsi na kuhakikisha miradi yenye athari kubwa inatekelezwa,” alisema.
Mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za fedha na wadau wa sekta binafsi ulijikita katika namna mbinu bunifu za kudhibiti hatari zinavyosaidia miradi kupata ufadhili kwa gharama nafuu na kirahisi.
Kwa uoande wake, Mtendaji Mkuu wa ATIDI, Manuel Moses, alisema kushughulikia athari ni muhimu kwani unafungua fursa za uwekezaji barani Afrika.
Moses alisema kuwa mitaji haiwezi kuingia kwa kiwango kikubwa bila mifumo madhubuti ya kudhibiti athari zake.
“Changamoto kubwa barani Afrika si ukosefu wa fursa bali ni athari za kiuwekezaji. Bila zana sahihi za kuzisimamia, mitaji haiwezi kutiririka kwa kiwango kikubwa. Hilo ndilo pengo ambalo ATIDI inalenga kuliziba,” alisema Moses.
Aliongeza kuwa Tanzania, ikiwa miongoni mwa nchi waanzilishi wa ATIDI, inaendelea kuwa soko la kimkakati katika kuchochea biashara na uwekezaji ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Kwa kupunguza mitazamo ya hatari na kuimarisha imani ya wawekezaji, ATIDI inasaidia kuelekeza mitaji katika miradi ya miundombinu, nishati na sekta binafsi, ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu na ushirikiano wa kikanda.
Naye Mwakilishi Mkazi wa ATIDI nchini, Tusekile Kibonde, alisema taasisi hiyo haijishughulishi tu na bima bali pia inasaidia wadau kubadili mtazamo kuhusu hatari katika uwekezaji.
“Kwa kusaidia serikali, wakopeshaji na wawekezaji kutazama upya hatari, tunawezesha upatikanaji wa fedha na kusaidia miradi inayotoa matokeo halisi kiuchumi na kuimarisha uunganisho wa kikanda. Nchini Tanzania, ushirikiano huu unatafsiri fursa kuwa ukuaji endelevu,” alisema.
ATIDI ilianzishwa mwaka 2001 kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) pamoja na Benki ya Dunia, na imekua taasisi kubwa zaidi barani Afrika inayotoa bima ya mikopo ya biashara na uwekezaji.
Hadi sasa ATIDI imeunga mkono zaidi ya dola bilioni 93 katika uwekezaji na biashara za kuvuka mipaka.
Alisema kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee kama mwanachama mwanzilishi wa ATIDI, ambapo miradi yenye thamani ya dola bilioni 7.8 imeungwa mkono huku kiwango cha hatari kinachobebwa kikifikia karibu dola bilioni 1.8.
Aliongeza kuwa msaada huu unahusisha sekta muhimu zikiwemo miundombinu, nishati, mawasiliano na makazi nafuu.
Miongoni mwa miradi mikubwa iliyoungwa mkono ni Reli ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR), ambayo imeboresha kwa kiasi kikubwa usafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma, kupunguza muda wa safari hadi chini ya saa nne, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji kikanda.
Mradi huo pia umechangia kupunguza hewa ukaa, kuunda ajira na kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na masoko ya nchi jirani.