
Dar es Salaam. Watanzania sasa wana fursa ya kupata matibabu ya kisasa ya kiwango cha kimataifa nje ya nchi kwa gharama nafuu, kufuatia ushirikiano wa makampuni matatu makubwa katika sekta ya bima na afya.
Makampuni hayo ni AXA Health International, Alliance Insurance Corporation Limited na MIC Global Risks Tanzania Ltd.
Afisa Mkuu Uendelezaji wa Biashara wa AXA Global Healthcare, Karim Idilby alisema kuwa wameamua kupanua wigo wa kutoa huduma za afya nchini kutokana na kutambua kuwa kuna uhitaji wa huduma hiyo kwa Watanzania wanapotakiwa kwenda nje kwa ajili ya matibabu.
Alisema kuwa matibabu ya nje ya nchi yana gharama kubwa na kusababisha wagonjwa wengi kushindwa kuyapata na kuwafanya wao kuunganisha nguvu kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Alifafanua kuwa gharama za wagonjwa kutibiwa nje zinatofautiana kutokana na sababu mbalimbali ikiwa pamoja na ugonjwa wenyewe, lakini wao wamekuja na suluhisho katika changamoto hizo.
“Kuanzisha ushirikiano huu nchini Tanzania ni hatua kubwa katika kuimarisha uwepo wetu katika masoko yenye ukuaji wa kasi na kuonyesha dhamira yetu ya muda mrefu barani Afrika,” alisema.
Alisema kuwa kadri Tanzania inavyozidi kuwa kitovu cha uwekezaji na biashara, ndivyo mahitaji ya huduma za afya za kimataifa yanavyoendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Alliance Insurance Corporation Limited, Rajiv Kumar, alisema kuwa ushirikiano huo unakuja wakati muafaka kufuatia mabadiliko ya mahitaji ya soko.
“Kadri uchumi wa Tanzania unavyokua na watu wengi kusafiri kimataifa, hitaji la huduma bora na za kuaminika za afya ya kimataifa linaongezeka. Ushirikiano huu unatoa suluhisho muhimu kwa wateja wetu,” alisema.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa MIC Global Risks, Aly Maherali, alisema mpango maalum wa afya wa watendaji wa kimataifa (GEHP), unatoa fursa kwa watu binafsi na makampuni kupata huduma ya afya wa kiwango cha kimataifa.
“Kwa uzoefu wetu wa zaidi ya miaka 25 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ushirikiano huu unaimarisha dhamira yetu ya kutoa huduma bora za bima zinazounganisha utaalamu wa ndani na viwango vya kimataifa,” alisema.
Alisema kuwa kwa sasa, AXA Global Healthcare inahudumia wateja katika zaidi ya nchi 200 duniani, ikiwa na mtandao wa zaidi ya watoa huduma za afya milioni 2.1 pamoja na huduma mbalimbali ikiwemo mashauriano ya mtandaoni, maoni ya pili ya kitabibu, usimamizi wa kesi na huduma za uokoaji wa kimatibabu.
Aliongeza kuwa ushirikiano huu unabadilisha taswira ya upatikanaji wa huduma za afya za kimataifa nchini Tanzania na kuweka viwango vipya katika utoaji wa huduma za afya zinazovuka mipaka.
“Ushirikiano huu unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za kitabibu za hali ya juu katika hospitali zinazotambulika kimataifa, sambamba na kupunguza gharama zinazoweza kuwa kikwazo kwa wengi, hivyo kuwapa Watanzania nafasi ya kunufaika na huduma bora za afya popote duniani,” alisema.