Marekani. Gari maarufu lililotumiwa na marehemu mwigizaji, Paul Walker kwenye filamu ya 2 Fast 2 Furious limeonekana tena hadharani baada ya kuhifadhiwa kwa takribani miaka 18.  

Gari hilo aina ya Nissan Skyline GT-R R34, lenye rangi ya silva na bluu, lililokuwa limehifadhiwa Barani Ulaya. Ni miongoni mwa magari yaliyotumika kama “hero car” wakati wa utengenezaji wa filamu hiyo, likimaanisha lilitumika kwenye matukio muhimu na kuonekana sana kwenye filamu hiyo.

Kwa mujibu wa kampuni ya Chromecars, wao ndio waliligundua gari hilo, likiwa limehifadhiwa na mmiliki binafsi. Inadaiwa kuwa mmiliki huyo alikuwa amelihifadhi ndani ya nyumba yake, jambo lililochangia kulifanya libaki katika hali yake ya awali bila kufanyiwa mabadiliko yoyote.

Hilo ni tofauti na magari mengi yanayotumika kwenye filamu ambayo hufanyiwa marekebisho kama kubadilishwa rangi au spea. Gari hilo lililotumiwa na Paul Walker limebaki katika hali ileile kama lilivyokuwa wakati wa kurekodi filamu, jambo lililofanya kuwa kumbukumbu adimu kwa mashabiki.

Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kumalizika kwa filamu, gari hilo lilipelekwa katika makumbusho ya Volo Auto Museum nchini Marekani. Baada ya muda liliuzwa kwa tajiri mmoja mwaka 2008, kisha kupelekwa nchini Norway ambako mmiliki alilihifadhi nyumbani kwake.

Aidha gari hilo limethibitishwa kuwa lenyewe na Craig Lieberman, ambaye alikuwa fundi wa magari yote yaliyotumika katika kurekodi filamu ya 2 Fast 2 Furious. Akieleza kuwa bado hajapoteza kumbukumbu, gari hilo ndio lenyewe ambalo lilitumiwa na Walker.

Paul Walker alifariki dunia Novemba 30, 2013 baada ya kupata ajali ya gari huko Santa Clarita. Amefariki akiwa na umri wa miaka 41.

Kifo chake kilisababisha huzuni kubwa kwa mashabiki na tasnia ya filamu. Huku kumbukumbu yake ikibaki hai kupitia kazi zake mbalimbali ikiwemo filamu ya Fast & Furious. 

Filamu hizo zilimpa umaarufu kimataifa na kumfanya kuwa moja wa nyota wakubwa wa tasnia ya filamu wanaofanya vizuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *