KAMPUNI za Afric Media Group na Genesis Entertainment Agency kutoka Cameroon zimefanya leo onesho la makala fupi iitwayo Universal Justice Without Universality, inayolenga kuangazia masuala ya haki za kimahakama barani Afrika.
Makala hiyo, iliyowasilishwa na Junior Wafo, inachambua jinsi mifumo ya haki ya kimataifa inavyofanya kazi, ikitumia mfano wa International Criminal Court (ICC). Inabainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo, kesi nyingi zimekuwa zikihusisha mataifa ya Afrika, jambo linalozua mjadala kuhusu usawa wa utoaji wa haki katika ngazi ya kimataifa.

Zaidi, makala hiyo imeibua hoja kuwa baadhi ya hukumu zimeonekana kuwa na athari kwa viongozi wa Afrika jambo linalochochea hitaji la bara hilo kujenga mifumo imara ya ndani ya kushughulikia changamoto zake za kisheria na kijamii. SOMA: Filamu ya ICC kuzinduliwa Dar, yazua mjadala wa haki ya kimataifa
Filamu hiyo pia imechochea wadau wa sanaa nchini kuanza kufikiria uzalishaji wa filamu za ukombozi zitakazolenga kuelimisha, kuunganisha, na kuhamasisha mshikamano wa Waafrika. Wadau hao wanaamini kuwa kupitia sanaa, hasa filamu, Afrika inaweza kuimarisha sauti yake na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayoihusu.