
Dar es Salaam. COSOTA, taasisi ambayo inashughulika na maswala ya hakimiliki, katikati ya mwezi huu ilitoa tamko ambalo nadhani ingefaa lirudiwe tena ili taarifa isambae zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya COSOTA, kumekuwa na wimbi kubwa la usambazaji wa kazi za muziki kupitia makundi ya Whatsapp. Yapo hata makundi ambayo yanaanzishwa kwa ajili tu ya kusambaza kazi za muziki.
Hakika hili si jambo la kushangaza kwani kwa sasa umekuwa ni utamaduni wa kawaida kwa shughuli hiyo kufanyika katika makundi ya whatsapp na Telegram.
Kuna watu ambao wanatambulika kwa majina kwa kuwa na uwezo wa kusambaza nyimbo kwa wingi katika makundi ya WhatsApp. Kitu kipya ni taarifa iliyotolewa na COSOTA kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki , Sura ya 218 ya Marejeo ya mwaka 2023, usambazaji huo usio halali unaweza kusababisha msambazaji akakabiriwa na adhabu ya faini au kifungo au vyote viwili kwa kosa hilo, maadmini wa makundi kaeni chonjo.
Na katika tamko hilo, COSOTA imewahimiza wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria, wahenga walisema mjumbe hauwawi.
Makala yangu ni kuhusu wanamuziki wenyewe kwa wenyewe kuibiana vipande vya nyimbo. Katika miaka ya karibuni kumekuweko na utunzi wa muziki kwa kutumia mtindo ulioitwa ‘sampling’.
Katika utunzi huo, sehemu ndogo ya wimbo huchukuliwa, sehemu hiyo huitwa ‘sample’ na hutumiwa kutunga nyimbo mpya.
Mara nyingi nyimbo iliyotengenezwa vizuri kwa sampling, huwa ngumu hata mwenye wimbo kugundua kuwa wimbo mpya anaousikiliza umetengenezwa kutoka kwenye wimbo wake.
Lakini nyimbo kadhaa hapa kwetu ambazo zinadaiwa zimetengenezwa kwa ‘sampling’, ziko wazi kabisa kuwa zimenyofolewa kutoka wimbo gani, hivyo hizo si sampling tena bali ni copying.
Kuna wasanii wakubwa duniani wamejikuta wakilipa fidia kubwa baada ya sampling kuzidi na kuonekana kuwa walichofanya ni kukopi tu sehemu ya kazi ya mtu mwingine
Ni swala la muda tu, kesi zitaanza kusikika za wizi wa vipande vya nyimbo kwani nyimbo nyingi maarufu za wasanii hapa nchini zimekuwa zikidokoa nyimbo za wanamuziki wengine bila kujali kutafuta ruksa rasmi.
Kwa kawaida kutumia kipande cha wimbo bila ruksa ya mwenye wimbo, kwanza huonyesha dharau ya kutoheshimu watunzi wa awali, pili ndipo linapokuja swala la kudai fidia ya matumizi ya kazi bila ruksa, ambapo anaedai huwa katika nafasi ya kudai fidia kubwa kadri ya anavyoona yeye anastahili kulipwa.
Lakini si mara ya kwanza duniani hili linatokea, tena kwa wanamuziki wenye majina makubwa duniani. Hebu tuangalie mikasa iliyowahi kutokea huko Magharibi.
Muimbaji Ed Sheeran alijikuta akidaiwa fidia ya ya dola 20milioni kutokana na wimbo wake unaoitwa Photographs, wimbo huo ulidaiwa kuwa ni wa kujaradia wimbo wa Matt Cardle unaoitwa Amazing, ulioachiwa mwaka 2009.
Amazing uliandikwa na Martin Harrington na Thomas Leonard. Mwanasheria wa watunzi hawa alikuwa Richard Busch, ambaye aliwahi kuitetea familia ya muimbaji Marvin Gaye katika kesi yao ya kudai haki za wimbo wa Marvin Gaye mwaka 2013.
Katika kesi hiyo ya Sheeran, inasemekana kwenye chorus nyimbo hizo mbili zinafanana kwa nota 39. Kwa maelezo yanayosema ‘ the notes are identical in pitch, rhythmic duration, and placement in the measure’.
Pia maelezo yaliyopelekwa mahakamani yanasema kuwa nyimbo hizo. Photograph na Amazing, zimefanana hata katika staili ya uimbaji, melodia ya uimbaji, mapigo au mkong’osio pia vinafanana.
Kundi maarufu la Beatles liliwahi kusimamishwa mahakamani na kampuni ya Big Seven iliyokuwa iki’publish’ nyimbo za mpiga gitaa Chuck Berry kwa kosa la la kutumia baadhi ya mistari kutoka wimbo wa You can’t touch me wa Chuck Berry na kutengeneza wimbo wao wa Come together.
Wimbo wa Chuck Berry ulitungwa mwaka 1956 na kesi ilikuja funguliwa mwaka 1973. John Lennon wa Beatles alikiri kuwa aliuitumia wimbo wa Chuck Berry kumpa hisia tu ya kutunga wimbo wa Come together. Hatimaye walikubaliana nje ya mahakama kuwa Lennon arekodi nyimbo 3 za kampuni Big Seven. Do Ya Think I’m Sexy?
Ulikuwa wimbo maarufu wa mwanamuziki Rod Stewart, lakini alipobanwa aeleze ukweli alikubali kuwa wimbo huo chanzo chake ni wimbo a mwaka 1979, Taj Mahal uliokuwa mali ya mwanamuziki wa Brazil Jorge Ben. Ben alipoenda mahakamani Stewart alikubali kutoa sehemu ya pato la wimbo huo kwa UNICEF.
Kundi la Radiohead la Marekani liliachia wimbo lililouita Creep, lilichukua melody ya wimbo wa miaka ya 60 wa kundi la The Hollies ulioitwa The Air that I breath, wapenzi wa muziki wakagundua mapema kuwa melody hiyo ni ya wizi, wakawataarifu waandishi wa awali wa wimbo huo, Hammond na Mike Hazelwood. Jamaa wakaenda mahakamani, na ikalazimika wakubaliwe kuwa nao ni sehemu ya watunzi wa wimbo huo mpya na lazima wapewe mgao wa mirabaha.
Rapa Jay Z nae alishtakiwa kwa kuiba vipande vya filimbi vilivyokuwemo katika wimbo wa Khosara uliorekodiwa mwaka 1957 Misri ukiwa utunzi wa Marehemu Hafez na Hamdy.
Jay Z akatumia vipande hivyo kwenye wimbo wake wa 1999 aliouita “Big Pimpin”. Jay Z alishinda kesi hiyo, lakini baadae yeye na Timbaland walidai walilipia Pauni 66,000 mwaka 2001, kwa kampuni ya EMI Music Arabia ili kupata leseni ya kutumia wimbo huo. Cha kujifunza hapa ni kuwa unaweza kudaiwa miaka mingi baada ya kuuachia wimbo uliou sempo.