Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Mpira wa Kikapu Afrika (Bal) wameanza vyema kupeperusha bendera ya nchi baada ya kuibuka na ushindi wa pointi 100-70 dhidi ya Johannesburg Giants katika mchezo uliochezwa jana Ijumaa, Machi 27, 2026 katika Uwanja wa SunBet Arena, Pretoria, Afrika Kusini.

Dalili za Dar City kutamba kwenye mchezo huo, zilionekana mapema katika robo ya kwanza ambapo ilimaliza ikiwa kinara kwa pointi 31 dhidi ya 12 za wenyeji.

Mambo yaliiendea vizuri Dar City katika robo ya pili ambapo ilivuna pointi 26 huku Johannesburg Giants wakipata pointi 18 jambo lililofanya wawakilishi hao wa Tanzania kumaliza nusu ya kwanza wakiwa na ushindi wa pointi 57-30 dhidi ya wapinzani wao.

Nusu ya pili ya mchezo ilianza vyema kwa Dar City kuongoza robo ya tatu kwa pointi 24-20 lakini robo ya mwisho haikuiendea vizuri kwani wenyeji walishinda kwa pointi 20-19.

Aliyeteka shoo ya jana ni Nisre Zouzoua wa Dar City ambaye alifunga pointi 35, akidaka mipira iliyorudi mara tano huku akitoa pasi moja iliyozaa pointi.

Baada ya ushindi huo, kibarua kinachofuata kwa Dar City ni leo, Jumamosi, Machi 28, 2026 itakapokabiliana na Nairobi City Thunder ya Kenya.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.

Ushindi katika mchezo huo utaiweka Dar City katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *