Mbeya. Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeanzisha mfumo maalumu wa ukusanyaji taarifa za siri ili kudhibiti vitendo vya uchakachuzi wa mbolea vinavyodaiwa kuongezeka na kuhatarisha sekta ya kilimo nchini.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara wasio waadilifu kuchakachua mbolea na kuwauzia wakulima, hali inayodhoofisha uzalishaji na kuathiri uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza Machi 27, 2026 katika mkutano wa wadau wa kahawa Kanda ya Mbeya, Meneja wa TFRA Kanda hiyo, Joshua Ng’ondya aamesema mamlaka imejipanga kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Amesema mfumo huo unahusisha ufuatiliaji wa mwenendo wa mauzo ya mbolea kwa wafanyabiashara wanaotiliwa shaka, pamoja na mtandao mpana wa taarifa za siri kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“Uchakachuzi wa mbolea ni hujuma inayodhoofisha juhudi za wakulima na kuathiri uchumi wa Taifa. Tumeweka utaratibu imara wa kuwabaini wahusika na tutachukua hatua kali ikiwamo kuwafungulia mashtaka ya uhujumu uchumi,” amesema Ng’ondya.

Amewataka wafanyabiashara kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya sekta hiyo, huku akiwahimiza wakulima kutoa taarifa wanapobaini uuzwaji wa mbolea nje ya mfumo rasmi.

Kwa upande wake, Ofisa Mdhibiti Ubora wa Mbegu kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), Laurent Mfagavo amesema wanaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa mawakala, maghala na mipakani ili kuhakikisha mbegu zinazowafikia wakulima zinakidhi viwango.

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wakulima ili waweze kutambua mbegu halisi na bora. Tunashirikiana na serikali za mitaa kuhakikisha mbegu zote zinazosambazwa zinakidhi ubora unaotakiwa,” amesema.

Naye Meneja wa Bodi ya Kahawa Kanda ya Mbeya, Ezekiel Mwakyoma amesema mkutano huo umejikita kujadili fursa na changamoto za zao la kahawa kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo.

Amesema maandalizi hayo ni sehemu ya kuelekea mkutano mkuu wa wadau wa kahawa utakaofanyika jijini Dodoma, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wenye tija katika mnyororo mzima wa thamani.

“Tunalenga kuona mkulima anazalisha kwa wingi na kwa tija. Pia tunaendelea na miradi ya matengenezo ya visima kwa ajili ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji,” amesema.

Baadhi ya wakulima walioshiriki mkutano huo walieleza umuhimu wa kudhibiti uchakachuzi wa mbolea ili kuongeza tija ya kilimo.

Mkulima Alex Mkumbwa amesema mafunzo wanayopata yameongeza uelewa wao katika kilimo cha kahawa, akibainisha kuwa bei ya zao hilo imekuwa ya kuridhisha msimu huu.

“Tunauza kahawa kupitia AMCOS kwa Sh9,000 hadi Sh12,000 kwa kilo. Elimu zaidi inahitajika ili tuendelee kuzalisha kwa ubora na kulinda thamani ya zao,” amesema.

Kwa upande wake, Yusuph Benson amesema licha ya jitihada hizo, bado wakulima wa vijijini wanakabiliwa na gharama kubwa ya mbolea kutokana na changamoto za miundombinu.

Amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti dhidi ya uchakachuzi utasaidia wakulima kupata faida na kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *