Dar es Salaam. Wajasiriamali nchini Tanzania, wamehimizwa kutumia fursa ya kusajili bidhaa zao kupitia QR code ili kujitangaza na kuongeza upatikanaji wa taarifa za kibiashara.

Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya GS1 Tanzania, Fatma Kange ametoa wito huo  leo Jumamosi Machi 28, 2026 katika mafunzo ya matumizi ya barcode  za 2D  kwa wajasiriamali na kuongeza kuwa, kupitia teknolojia hiyo, wajasiriamali wanaweza kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa, ikiwamo Afrika Mashariki, huku wakichangia kukuza uchumi wa kidijitali.

Aidha, amesema GS1 ipo katika mpango wa kuanza matumizi ya barcode za 2D ifikapo mwaka 2027, hatua itakayoboresha mfumo wa sasa wa barcode za 1D ambazo zimetumika kwa miaka 15, lengo ni kuwezesha uwekaji wa taarifa nyingi zaidi za bidhaa na kurahisisha ufuatiliaji wake katika soko la dunia.

“Miaka 15 baadaye  teknolojia ya barcode imebadilika, tupo kwenye maandalizi ya kuelekea kuzindua mpango huu Septemba 30 mwaka huu, teknolojia hii ni maandalizi ya uchumi wa kidijitali  na uhamasishaji wa matumizi ya barcode za 2D ikiwa ni sehemu ya kuelekea miaka 15 ya GS1,  hivyo lazima tuangalie bidhaa za Tanzania zinashiriki vipi katika uchumi wa kidijitali na zinanufaika vipi,” amesema.

Wajasiriamali wakiwa kwenye mafunzo ya teknolojia ya barcode za 2D  yanayotolewa na Taasisi ya GS1 Tanzania, jijini Dar es Salaam leo Machi 28, 2026

Amesema ujio wa barcodes za 2D kwa wafanyabiashara ni fursa nyingine ya kujitangaza zaidi kwa kuhakikisha taarifa zao zilizopo instagram, facebook na mitandao mingine ya kijamii  zinajulikana na bidhaa kuwa rahisi kupatikana.

“Kama kwa siku  mjasiriamali  simu  yako haiingizi Sh5,000 umefeli,  hivyo wakati umefika wa kutumia teknolojia na kuingia kwenye uchumi wa kidijitali ili bidhaa ipate thamani katika soko,” amesema.

Akitolea mfano wa mabadiliko amesema zamani bidhaa kama asali zilikuwa zinapakiwa kwenye chupa zilizoisha  pombe lakini sasa inapakiwa kwenye vifungashio maalumu na kuvutia wateja.

Mmoja wa wajasiriamali Mwavita Ramadhani, amesema awali kabla hajaanza kutumia QR Code ilikuwa vigumu kupata wateja na hata alipokwenda kwenye maduka makubwa (super market) aliambiwa bidhaa yake lazima iwe na taarifa muhimu ndio apate fursa.

“Baada ya kujisajili na QR Code  na barcode za 1D biashara imekua na hata wateja napata,  kwa hiyo huu ujio wa  barcode za 2D, naimani biashara yangu itakua zaidi, nitauza Kenya, Uganda na mataifa mengine,” amesema Mwamvita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *