Chanzo cha picha, Reuters
Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Iran wamejadili uwezekano wa kumaliza mzozo unaoendelea kwa njia ya kidiplomasia, huku wakisisitiza umuhimu wa suluhisho la kisiasa katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alifanya mazungumzo na mwenzake wa Iran, Abbas Araqchi, kuhusu namna ya kuhamisha mzozo huo kutoka uwanja wa kijeshi kwenda kwenye mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia (Reuters).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya mambo ya nje ya Urusi, mawaziri hao walijadili kwa kina hali ya kisiasa na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, wakieleza kuwa mgogoro huo umetokana na kile walichokiita uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Pia walibadilishana mawazo kuhusu uwezekano wa kufikia suluhisho la kudumu kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maslahi ya nchi zote katika ukanda huo.
Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa Urusi imewasilisha misaada ya kibinadamu nchini Iran kama sehemu ya ushirikiano wao wa kimkakati unaojumuisha sekta za siasa, uchumi, kijeshi na nishati. Hata hivyo, makubaliano hayo hayajumuishi ulinzi wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.
Wakati huo huo, Mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya walitumia mkutano wa G7 kumueleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa Urusi inashutumiwa kusaidia Iran kulenga majeshi ya Marekani katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.