
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema mashambulizi mapya ya Ijumaa kwenye vituo vya amani vya nyuklia nchini Iran yanapasa kulaaniwa kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, mashambulizi mapya dhidi ya vituo vya amani vya nyuklia nchini Iran siku ya Ijumaa yanapasa kulaaniwa kimataifa, na kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa na msimamo wa wazi na kubainisha bayana kwamba wavamizi wa Marekani na Wazayuni wamevuka mipaka.
Maria Zakharova ameongeza katika taarifa yake ya Jumamosi kuwa: “Wavamizi dhidi ya Iran wanaendelea kuzidisha mvutano katika vita vyao vya Asia Magharibi, wakipuuza hatari zote zinazoweza kutokea, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuenea kwa uchafuzi wa mionzi.”
Taarifa hiyo imesema: “Siku ya Ijumaa, pande zilizoishambulia Iran zilifanya mashambulio yaliyolenga eneo la maji mazito huko Khandab na kiwanda cha uzalishaji wa madini ya uranium huko Ardakan. Mara tu baada ya hapo, kulikuwa na ripoti za mashambulio mapya katika eneo la kiwanda cha nyuklia cha Bushehr.”
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amesema: “Tunatumai kwamba Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, kwa kupokea haraka ripoti kuhusu hali halisi ya mambo moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa Iran, ataweza mara moja na kwa uwazi kufikisha ujumbe huu rahisi kwa wavamizi kwamba: ‘Wakati wa kusimamisha mashambulizi umefika! Mmevuka mstari mwekundu, lakini bado mna fursa ya kuzuia jinai zaidi, ongezeko la wahanga wasio na hatia na kuzuia maafa haya kuwa janga la kimataifa.'”