
Dar es Salaam. Kifo cha mwanasiasa mkongwe, Selemani Bungara, maarufu Bwege aliyewahi kulitikisa Bunge kwa hoja zake na kauli zilizokuwa zikivuma mitandaoni, kimewastua wengi.
Bwege aliyewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kusini kuanzia mwaka 2010 hadi 2020 kupitia Chama cha Wananchi (CUF), alijizolea umaarufu ndani na nje ya nchi kutokana na misimamo yake na kauli yake maarufu aliyopenda kuitumia ya ‘tunaanza upya’ na ile ya ‘valangati lilelile.’
Kauli hizo zilimfanya abaki kwenye kumbukumbu za wengi kama kiongozi jasiri na asiyeogopa kusema ukweli lakini hata alipokuwa nje ya muhimili huo wa Bunge, bado aliendeleza kauli zake za kupigania mageuzi ya kweli ya kisiasa nchini.
Mwanasiasa huyo aliyekuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo, kabla ya Februari 18, 2026 kutangaza kujiondoa na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), sasa amelala usingizi wa milele.
Amefariki dunia leo Jumatatu Machi 30, 2026 katika Hospitali ya EM iliyopo Mji Mwema, Kigamboni, jijini Dar es Salaam alikokuwa akisubiri kupatiwa matibabu ya usafishaji wa figo ‘dialysis.’
Kwa mujibu wa ndugu yake, Nasri Omari, aliyekuwa naye hospitalini hapo, hali ya Bwege ilibadilika ghafla kabla ya kuanza kupatiwa huduma hiyo.
“Amefariki wakati akisubiri kupata matibabu ya dialysis… kabla huduma hazijaanza, hali yake ilibadilika na kufikwa na umauti. Amefariki majira ya saa saba mchana,” amesema.
Hata hivyo, Omari amesema maziko ya mwanasiasa huyo mkongwe yatafanyika kijijini kwa Kilwa mkoani Lindi kesho Jumanne Machi 31, 2026.
Wadau wa siasa wamzungumzia
Wakimzungumzia mwanasiasa huyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamemtaja kama mwanasiasa shupavu, aliyekuwa na msimamo usioyumba na aliyeonyesha kwa vitendo maana halisi ya uwakilishi wa wananchi.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema wamepokea taarifa za kifo chake kwa masikitiko makubwa.
“Alisimama na watu wote bila kujali, alikuwa tayari kuhoji na kueleza mawazo yake. Siasa ilikuwa kwenye damu yake kwa sababu hata wakati wa kuugua kwake aliendelea kushiriki katika siasa na ujenzi wa chama chake,” amesema.
Amesema Bwege alikipenda chama cha ACT- Wazalendo sambamba na wananchi wa Kilwa, na siku zote alikuwa tayari kuzungumzia masuala yanayohusu wananchi bila hofu.
“Alipenda kuishi na watu waliomchagua na alifanya jitihada zote kuwasemea. Hata mwezi mmoja uliopita alikwenda Kilwa kufuatilia kesi ya eneo la chama,” amesema.
Semu amesema Bwege atabaki kwenye kumbukumbu za ACT-Wazalendo kama mwanasiasa wa kuigwa, kwa kuwa alikuwa kinara wa kusemea masuala ya wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa amesema wamesikitishwa na kifo chake kwa sababu walikuwa katika hatua za mwisho za kumkaribisha kujiunga na Chadema.
“Akiwa hai, aliwahi kuniita nyumbani kwake akanieleza nia yake ya kujiunga na Chadema baada ya wananchi wa Kilwa kumwambia kuwa hawana imani na chama alichokuwemo, kwani hakiwezi kusimamia mageuzi ya kweli,” amedai.
Golugwa amesema alipoitwa aliitikia wito huo na kwenda kufanya naye mazungumzo marefu, na alimweleza nia yake ya kutaka kujiunga na Chadema.
“Tulikubaliana baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tungefanya ziara maalumu ya kwenda Kilwa kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya, akiwamo yeye rasmi. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mauti yamemkuta,” amesema kiongozi huyo.
Hata hivyo, amemuelezea Bwenge kama mwanasiasa aliyeuwa amebeba taswira halisi ya maana ya uwakilishi wa wananchi.
“Akiwa bungeni, ukimsikia akizungumza, ilikuwa ni wazi anawakilisha sauti na vilio vya wananchi. Aliuvaa ubunge na kuutumikia kwa masilahi ya umma,” amesema kiongozi huyo.
Golugwa anasema Bwenge aliamini katika kufanikisha mabadiliko makubwa ya kimfumo, yatakayowezesha maendeleo ya wananchi, upatikanaji wa katiba mpya na kujengwa kwa Taifa lenye haki.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya amesema Bwege mara zote alikuwa ni mtu wa msimamo usioyumba, lakini pia jasiri asiyeogopa.
“Ilikuwa hata akisimama bungeni enzi zile au katika vikao vya chama, alikuwa akizungumza kwa msisitizo na kupenda mambo yanayojadiliwa yatekelezwe,” amesema.
Amesema ni miongoni mwa wanasiasa waliokipenda chama ndiyo maana aliibeba CUF mabegani mwake muda wote alipokuwa mwanachama wa chama hicho.
“Hata alipohamia ACT – Wazalendo, alitumia ngome ya kusini kukijenga chama hicho,” amesema Sakaya.
Amesema kupungua kwa ushawishi wa CUF katika mikoa ya kusini kulichangiwa na Bwege kukihama chama hicho, kwa sababu alikuwa anaimarisha ngome hizo na kuzifanya ziwe za ACT – Wazalendo.
“Bwege alikuwa mpambanaji; hata ukienda kwenye wilaya yake unajivunia. Watu wake walikuwa wanampenda na alipenda siasa za kweli bila unafiki,” amesema.