Majukumu hayo yanatokana na maamuzi ya nchi wanachama —  yanapitishwa, yanatekelezwa na kufanyiwa tathmini kupitia mfumo mzima.

Hatua hii ni kiashiria cha aina yake chini ya Mpango wa Umoja wa Mataifa kutimiza miaka 80, au UN80 Initiative, amba oni jitihada kubwa za Umoja wa Mataifa za kuelekea kuwa fanisi zaidi, kujiratibu vema, kuwa na nyenzo sahihi na kujipanga vema kuleta matokeo katika dunia inayobadilika kwa kasi.

Akizungumza kwenye Ukumbi wa Baraza Kuu baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha hatua ya kupitishwa akisema, “ni azimio la kihistoria” na ni hatua kubwa.

“Azimio hili lililopitishwa leo linaakisi uelewa wa pamoja wa mzunguko mzima wa majukumu na wajibu wa UN – na ahadi ya pamoja ya kuimarisha kila hatua,” amesema Katibu Mkuu mbele ya wajumbe wa nchi wanachama.

“Hii leo azimio hili litasaidia kutafsiri kivitendo Mpango wa Utekelezaji wa Miaka 80 ya UN uliojaa matarajio makubwa.”

media:entermedia_image:07eacb4d-a5df-4fac-a1f9-120bfae90ebe

UN Photo/Rick Bajornas

Bendera za Taifa zikipepea nje ya jengo la Baraza Kuu wakati wa mjadala mkuu.

Kwa nini upangaji wa majukumu ni muhimu?

Kwa kupanga majukumu, nchi wanachama zinaelekeza na kuongoza mfumo mzima kuhusu jinsi ya kushughulikia changamoto za kimataifa: kuanzia kuimarisha amani na usalama na kutoa misaada ya kibinadamu, hadi kuendeleza maendeleo na kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo, kadri muda ulivyopita, idadi kubwa ya majukumu yalikumbana na changamoto za kiutendaji.

Tangu mwaka 1946, zaidi ya maazimio, maamuzi na matamko ya Rais 40,000 yamepitishwa katika vyombo vikuu vya Umoja wa Mataifa — hali ambayo inazidi kuwa ngumu kuielewa na kuisimamia.

Hali hii imesababisha:

  • Kurudiwarudiwa na kuingiliana kwa kazi,
  • Kuongezeka kwa ripoti na mikutano,
  • Ukosefu wa uwazi na mifumo ya tathmini katika mfumo mzima.

Hii inaweza kuweka mzigo mkubwa kwa nchi wanachama na mfumo wa Umoja wa Mataifa, huku ikifanya iwe vigumu zaidi kuhakikisha utekelezaji wa mamlaka kwa ufanisi na kwa tija.

‘Njia iliyo na muundo bora zaidi’

Azimio hili linaanzisha, kwa mara ya kwanza, mbinu iliyo na muundo bora zaidi katika mzunguko mzima wa mzunguko wa majukumu — kuanzia kubuni, utekelezaji hadi tathmini.

Kwa vitendo, hii inamaanisha:

  • Majukumu yaliyo wazi zaidi na zenye mwelekeo mahsusi, zikisaidiwa na taarifa bora kwa ajili ya maamuzi tangu mwanzo;
  • Utekelezaji ulioimarishwa na unaoratibiwa vyema zaidi, kwa kutumia data kwa ufanisi zaidi, ripoti zinazolenga watumiaji na matumizi bora ya rasilimali;
  • Tathmini ya kimfumo zaidi ya matokeo, kusaidia kuhakikisha majukumu yanaendelea kuwa na umuhimu na kutoa matokeo yenye Athari chanya, na kuimarisha utamaduni wa maboresho endelevu unaotegemea ushahidi, uwajibikaji na matokeo.
  • Kuongezeka kwa uwazi kupitia zana bora za kidijitali, ikiwemo kupanuliwa kwa Daftari la Majukumu ya Mataifa, ili kuwapa nchi wanachama taarifa zilizounganishwa na zinazolinganishika zaidi kuhusu majukumu, rasilimali na matokeo.

Kwa nini hili ni muhimu

Azimio hili linalenga kurahisisha kwa nchi wanachama kuuelewa mfumo unaozidi kuwa tata wa majukumu, huku likisaidia Umoja wa Mataifa kupunguza urudufu, mgawanyiko na kutokuwa na ufanisi.

Kwa kuimarisha namna majukumu yanavyobuniwa, kutekelezwa na kutathminiwa, linakusudia kuboresha jinsi mfumo wa Umoja wa Mataifa unavyogeuza maamuzi kuwa matokeo halisi.

Magari mawili ya silaha yaliyo na bendera na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa yanapita kwenye eneo la mashambani lenye milima na majengo yaliyotawanyika.

UN Photo EPPasqal Gorriz

Walinda amani wakipiga doris kwenye eneo la Blue Line

Hatua zinazofuata

Azimio hili linajengwa juu ya kazi ya Kikundi Kazi Maalum kisicho rasmi cha Baraza Kuu kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Majukumu, kinachoongozwa kwa pamoja na Jamaica na New Zealand.

Kikundi hicho kiliundwa na Baraza Kuu ili kuchambua mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya Katibu Mkuu ya Julai 2025 kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Majukumu, iliyoandaliwa chini ya Awamu ya Pili ya Mpango Kazi wa Mpango wa UN80.

Ripoti hiyo ilichunguza jinsi majukumu yanavyoundwa, kutekelezwa na kutathminiwa katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, na kutoa mapendekezo ya kuimarisha kila hatua ya mzunguko wa kipindi cha majukumu.

Azimio linaamua kuendeleza kazi hiyo kupitia Kikundi Kazi Maalum rasmi kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa Majukumu, ambacho kiko wazi kwa nchi wanachama wote na waangalizi.

Majukumu yake ni pamoja na, kwa mfano, kuandaa mifumo bora ya vitendo, vifungu madhubuti vya tathmini, na mapitio zaidi ya majukumu yaliyopo.

“Hii ni hatua kubwa. Lakini ni mwanzo tu. Tutafanya kazi kama Shirika moja lenye mshikamano — tukiongozwa na Kikundi Kazi — kuboresha jinsi mamlaka zinavyoungwa mkono na kutekelezwa,” amesema Guterres, akisisitiza kuwa huu unabaki kuwa mchakato unaoongozwa na nchi wanachama.

Akisisitiza hoja hiyo, Rais wa Baraza Kuu, Annalena Baerbock, amesema kupitishwa kwa azimio hilo ni hatua muhimu katika juhudi pana za mageuzi, na akazialika nchi wanachama kuendelea kushiriki katika hatua inayofuata ya kazi. “Leo tumepiga hatua muhimu kuufanya Umoja wa Mataifa uwe na wepesi zaidi, ufanisi zaidi, na uwezo mkubwa zaidi wa kukidhi mahitaji ya siku zijazo, ili uweze kuhudumia watu tunaowahudumia kwa ubora zaidi,” amesema.

Mpango wa UN80

Azimio hili ni hatua ya hivi karibuni katika Mpango wa UN80, ulioanzishwa na Katibu Mkuu mwaka mmoja uliopita, mpango huu unalenga kuleta mabadiliko katika Umoja wa Mataifa kwa ngazi zote, ili kila jukumu, dola inayotumika na kila uamuzi uwe na thamani ya juu kwa watu duniani.

Jumatatu ijayo, Baraza Kuu litafanya mkutano usio rasmi kupokea taarifa ya hivi karibuni kuhusu Mpango wa Hatua wa UN80, ikiwa ni pamoja na mapendekezo chini ya Awamu ya tatu ya Mpango Kazi unaobainisha uwezekano wa marekebisho ya kimuundo na kiprogramu ili kuoanisha vyema mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo utarushwa mubashara kupitia televisheni  ya mtandao ya Umoja wa Mataifa, UNWebTV.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *