
MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Paul Peter amesema bao lake la kwanza katika timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ limempa faraja na sasa anarejea kwa waajiri wake akiwa na lengo la kufunga zaidi ili kuendelea kuitwa Stars na kuboresha namba zake.
Hii ni mara yake ya kwanza kuitwa ndani ya kikosi cha timu ya Taifa, na kufanikiwa kufunga bao dakika ya 56 kwenye mechi dhidi ya Macau, ambapo Stars ilitoka na ushindi wa mabao 6-0.
Peter, ambaye aliwahi kuchezea Azam FC na KMC kabla ya kujiunga na JKT, mpaka sasa ni miongoni mwa washambuliaji wenye mabao mengi Ligi Kuu, akifunga matano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Peter alisema mafanikio hayo ni chachu mpya kwake kwani yalikuwa sehemu ya ndoto zake tangu alianza kucheza soka la ushindani, hivyo anajiona yupo kwenye njia sahihi ya kufikia malengo makubwa zaidi katika maisha yake ya soka.
Aliongeza kuwa ndani ya Stars kuna mazingira mazuri yanayowapa nafasi wachezaji chipukizi kuonyesha uwezo wao, jambo linalowafanya wajiamini zaidi wanapopata nafasi ya kucheza kwenye mechi za kimataifa.
“Uwepo wa kocha Miguel Gamondi ndani ya timu hii unanipa motisha kubwa kwani ni aina ya mwalimu anayependa kuona vijana wakipambana na kuonyesha viwango vya juu kila wanapopewa nafasi,” alisema Peter.
“JKT pia inanipa sapoti kubwa, hasa kutoka kwa benchi la ufundi likiongozwa na kocha Ally Hamad, ambaye amekuwa akiniamini kwa kiasi kikubwa na kunipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu uwanjani.
“Sitaki kuipoteza imani niliyopewa na makocha wote wawili, kwani naamini ndiyo msingi wa mafanikio yangu. Nitahakikisha naendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuwa kwenye kiwango bora.”
JKT Tanzania bado iko kambini Arusha, ambako wanaendelea kujinoa kwa ajili ya raundi ya pili ya ligi, huku wakiwa nafasi ya nne kwenye msimamo, baada ya kucheza mechi 17 na kufikisha pointi 28.