
WAKATI Tanzania Prisons ikiendelea kujifua kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga, kipa wa timu hiyo, Edward Mwakyusa, amesema mechi hiyo ni ya kufa au kupona katika kupambania pointi tatu.
Mwakyusa pia ametoa angalizo kwa wachezaji wenzake kutomkaba mtu mmoja, bali kila mmoja apambane kudhibiti mashambulizi ili kutoruhusu bao lolote.
Prisons inatarajia kushuka uwanjani kuwakabili vinara hao wa Ligi Kuu na bingwa mtetezi, katika mchezo utakaopigwa Aprili 4 jijini Dar es Salaam, ukiwa wa mzunguko wa pili.
Maafande hao wanawakabili Yanga wakiwa hawana matokeo mazuri wakiwa nafasi ya 15 wakimiliki pointi 13, wakicheza mechi 17, huku Yanga ikiongoza na pointi 38.
Mwakyusa anakumbukwa kuikoa timu hiyo kutoshuka daraja msimu wa 2022/23 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa play-off uliopigwa Sokoine na kumalizika kwa sare ya 1-1, na kufanya Prisons kubaki salama kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya ushindi wa awali ugenini wa bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwakyusa alisema matokeo waliyonayo siyo mazuri licha ya matumaini ya kufanya vizuri katika michezo zilizobaki, hivyo kwa sasa kila mechi kwao ni vita nzito ya pointi tatu.
Alisema kuwa wakati wakiendelea na mazoezi, akili zote zinaufikiria mchezo ujao dhidi ya Yanga, akieleza kuwa mkakati wao ni kufa au kupona kuhakikisha hawapotezi mechi hiyo muhimu kwao ili kujinasua kutoka nafasi za mkiani.
“Ni kufa au kupona. Yanga yeyote anakufunga, kwa hiyo hakuna sababu ya kumzuia mmoja, bali tudhibiti mashambulizi yote ili tusiruhusu bao. Tunajua ugumu wa mechi hiyo, lakini kwa umuhimu wake lazima tupambane,” alisema Mwakyusa.
Kipa huyo aliyeanza soka akicheza winga wa kulia, ameongeza kuwa licha ya kutopata nafasi ya kucheza anaamini muda ukifika ataonyesha uwezo kwa kuwa anajiamini na kipaji alichonacho, na anasubiri uamuzi wa kocha Shadrack Nsajigwa kuhusu hatma yake.
Kinda huyo mwenye utulivu awapo golini amekiri kuwapo kwa ushindani wa namba kikosini, akieleza kuwa uwezo mkubwa alionao kipa mwenzake, Mussa Mbisa, unamfanya kujifunza mengi ili atakapoaminiwa kupewa nafasi aweze kuisaidia timu hiyo.
“Matokeo yanatuumiza wote, lakini hatujakata tamaa, na matarajio yetu ni kwamba timu haishuki daraja wala kucheza play-off. Binafsi, naendelea kujifunza kwa mwenzangu aliyenitangulia nikiamini nitaisaidia timu yangu,” alisema.
Timu hizo zinatarajia kukutana huku Yanga ikiwa na rekodi nzuri, kwani mara ya mwisho Prisons kushinda dhidi ya wapinzani hao ilikuwa Mei 10, 2018 ilipotakata mabao 2-0, na tangu hapo imekuwa ikiambulia vipigo na sare katika mechi chache.